The House of Favourite Newspapers

JAMII ISIWADHARAU MAKONDAKTA WA KIKE

0

IMEZOELEKA kazi ya ukondakta hapa nchini Tanzania inafanywa na wanaume lakini kutokana na ugumu wa maisha na kuongezeka kwa majukumu, kazi hiyo kwa sasa inafanywa mpaka na wanawake.Hivi sasa wapo wanawake mbalimbali wanaofanya kazi kwenye daladala, jijini Dar es Salaam na mikoani, tena wanaifanya kikamilifu. Inaweza kuonekana kama ni jambo geni hapa nchini lakini nchi nyingine ni jambo lililozoeleka kabisa.
Awali ilikuwa vigumu kuamini kama siku moja itatokea wanawake wakafanya kazi hiyo lakini abiria, madereva, na wamiliki wa magari yanayotumika kama daladala, kwa sasa wana imani kubwa juu ya makondakta wa kike.

Kilichofanya niandike makala haya ni kutokana na nilichokiona leo asubuhi wakati natoka nyumbani kuelekea kibaruani kwangu, nikiwa ndani ya daladala inayotokea Segerea kwenda Makumbusho jijini hapa, tulipofika maeneo ya Mwenge ghafla nikasikia mzozo.
Ulikuwa ni mzozo kati ya kondakta wa kike wa gari nililokuwa nimepanda akibishana na mmoja wa abiria mwanaume ambaye aligoma bila sababu ya msingi kulipa nauli, jambo lililosababisha ugomvi, kutoleana kauli zisizofaa.
Ikafikia hatua wakataka hadi kupigana, kwa bahati nzuri ndani ya gari kulikuwa na abiria wenye busara, wakamaliza utata ule, yule abiria akakubali kulipa nauli na akashuka kituo kilichofuata ITV.
Moja kati ya kauli alizoziongea kijana yule ni “Wewe mwanamke utanifanya nini mimi, kwanza hizi kazi haziwafai ulitakiwa kukaa nyumbani unyonyeshe watoto!”

Nilijikuta nimepata simanzi na uchungu baada ya kusikia kauli ile inayomfedhehesha mwanamke.
Kauli mbiu ya Rais wetu John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu inasisitiza Watanzania wote kufanya kazi yoyote ile kwa bidii, ilimradi uheshimu katiba, usivunje sheria, sasa watu kama huyu abiria wanapingana na kauli kama hii.
Si vyema kuwadharau au kuwashushia heshima makondakta wa kike, kwani na wao wapo kwenye mchakato wa kutafuta riziki kwa ajili ya kusaidiana na waume zao kusukuma gurudumu la maisha na kujikwamua na umaskini, jambo ambalo siyo dhambi wala si vibaya, tena wanapaswa kuungwa mkono.

Jamii inapaswa kuelimishwa na ikubali kubadili mtazamo hasi juu ya makondakta wa kike, kitendo cha kuwakejeli na kuwakebehi , kitasababisha waache kazi hiyo warudi na kuwa magolikipa nyumbani.
Sijui tutamalizaje tatizo la watu wasio na ajira nchini, na vipi kuhusu pato la taifa litaongezekaje ikiwa walipa kodi hawafanyi kazi, tukiendelea na dhana hiyo potofu, kamwe tusitegemee kumaliza tatizo la umaskini.

Na Isri Mohamed/ GPL.

Leave A Reply