The House of Favourite Newspapers

Jinsi Mwanamke Anavyoweza Kujitambua Kama Hana Uwezo wa Kupata Ujauzito-2

WIKI iliyopita nilianza kuzungumzia mada hii na leo nitaimalizia. Tatizo lingine katika kizazi lipo kwenye mirija ya uzazi. Mirija ya uzazi ipo miwilini kwa mwanamke, mmoja kulia na mwingine kushoto. Kazi ya mirija wa uzazi ni kusafirisha mayai na kutungisha mimba.

 

Mimba inatungwa kwenye mrija halafu inasafirishwa hadi ndani ya kizazi ili ikue. Mirija ya kizazi ina sehemu kuu tatu, kwanza ni sehemu inayoungana na kizazi ambayo ni nyembamba, halafu sehemu ya kati ambayo ni pana, mwishoni mwa mirija ni vidole vyake vyenye kazi ya kuchukua yai lililokomaa na kuliingiza ndani ya mirija. Yai lisipokutana na mbegu hutoka na damu ya hedhi.

 

Matatizo kwenye mirija ni maambukizi yatokayo kwenye kizazi na kusambaa huko, mirija kukatwa kwa upasuaji wa kufanga kizazi au mimba kutungia kwenye mirija ‘Ectopic Pregnancy’.

 

Dalili za maambukizi ya mirija ya uzazi ni maumivu chini hya tumbo yanayosambaa kulia na kushoto, maumivu ya kiuno, maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo, maambukizi makali huweza kusababisha mgonjwa awe na homa. Athari za maambukizi ya mirija ni kuziba kwa mirija. Mirija inaweza kupoteza uwezo wake wa kutungisha mimba kama itakatwa, pia endapo itaharibika kwa maambukizi. Maambukizi ya mirija huweza kusababisha mirija iharibike kwa kujaa maji au kujaa usaha.

 

 

Vyanzo vingine vya matatizo yote haya ni kuharibika kwa mimba, iwe kwa bahati mbaya au kwa kuitoa kwa makusudi. Mirija kama imethibitika imeziba, basi ni vema umuone daktari bingwa wa kinamama ili aangalie jinsi ya kukusaidia. Vifuko vya mayai pia ni sehemu nyingine muhimu sana katika mfumo wa viungo vya uzazi vya mwanamke. Vifuko vya mayai vipo kulia na kushoto. Kazi ya ovari ni kupevusha mayai na kuzalisha vichocheo au homoni za Progesterone na Estrogen.

 

Homoni hizi ni muhimu katika mfumo wa uzazi wa mwanamke. Matatizo katika vifuko vya mayai ni kushindwa kuzalisha vichocheo hivyo kwa kiwango chake, uvimbe au Ovarian cyst, kutokwa na vivimbe vidogovidogo sehemu hiyo ya ovari viitwavyo Polycystic. Dalili za matatizo katika vifuko vya mayai ni kuvurugika mzunguko wa hedhi, kutokupata hedhi pasipokuwa mjamzito, maumivu upande mmoja chini ya tumbo. Tiba yake inaweza kuwa dawa au upasuaji endapo uvimbe huu ni mkubwa sana au umejinyonga.

 

MATATIZO YA MFUMO WA HOMONI

 

Hii ni sehemu nyingine kubwa ya pili inayosababisha mwanamke asifanikiwe kupata ujauzito. Mwanamke anaweza kuishi muda mrefu na mumewe bila mafanikio, mumewe akawa vizuri tu na yeye akajihisi hana tatizo lolote lakini mimba haipatikani. Matatizo ya mfumo wa homoni huambatana na baadhi ya dalili zifuatazo.

 

Kupata siku za hedhi bila mpangilio, kufunga kupata hedhi kwa muda mrefu, kutopata ute wa uzazi, kutohisi hamu au raha wakati wa tendo la ndoa, maziwa kutoka wakati huna mimba au hunyonyeshi, kujihisi mjamzito wakati huna mimba. Chanzo cha matatizo haya yote ni mengi na zaidi huwa ya muda mrefu. Ni vizuri umuone daktari bingwa wa matatizo ya uzazi au magonjwa ya kinamama katika hospitali ya mkoa.

Comments are closed.