The House of Favourite Newspapers

JUX, VANESSA WAUVAA MOTO WA SERIKALI

Juma Khalid ‘Jux’ na Vanessa Mdee ‘V-Money’

BAADA ya hivi karibuni kuonyesha mambo ya chumbani jukwaani na picha yao ya mahaba mazito kusambaa mitandaoni, wasanii wa Bongo Fleva ambao ni wapenzi, Juma Khalid ‘Jux’ na Vanessa Mdee ‘V-Money’ wamejikuta wakiuvaa moto wa serikali, Risasi Mchanganyiko linakujuza.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza alisema wao kama serikali picha hiyo imewachefua na hawajui ni shetani gani amewapata vijana hasa hao wanamuziki kwani kila kukicha wamekuwa wakionyesha vitendo visivyokuwa na maadili kwa jamii.

Mngereza alisema kuwa kutokana na picha hiyo lazima waifanyie kazi kwani kwa sasa hawawafumbii macho wasanii wanaokwenda kinyume na maadili na siku zote moto ni uleule.

“Sijui ni shetani gani amewaingia hawa vijana wanamuziki maana kila siku wanaonyesha vitu vya ajabu vizivyokuwa na maadili wanapokuwa jukwaani kwani hivi karibuni msanii Mbosso naye alifanya shoo na kuonyesha vitendo vilivyo kinyume kabisa na maadili, tukamuita na kumuonya na kumwagiza aombe msamaha kwa mashabiki na alifanya hivyo.

“Sasa huyu Jux na Vanessa hata kama ni wapenzi hawakutakiwa kufanya hayo waliyoonyesha jukwaani kwani kama ni mahaba mnatakiwa muonyeshane mkiwa faragha na siyo hadharani kama walivyofanya tunawafanyia kazi ili kukomesha tabia hizo,” alisema Mngereza.

ATOA TAMKO

Mngereza alitoa tamko kwa kuwataka wasanii kufanya mambo yanayoheshimu maadili na kuachana na tabia ya kuvunja maadili kila kukicha kwa kuonyesha mambo ya chumbani hadharani na wale watakaoendelea na uchafu huo wao kama serikali hawatasita kuwachukulia hatua kali.

Hata hivyo Mngereza aliwataka maafisa utamaduni waliopo katika kila mkoa kuangalia yale wanayoyafanya wasanii wanapokuwa kwenye shoo zao majukwaani na kuwachukulia hatua kuanzia ngazi ya wilaya hadi ngazi za juu na hilo litasaidia kutokomeza tabia hizo chafu zinazoibuka kwa sasa.

TUJIKUMBUSHE

Mwishoni mwa wiki iliyopita Jux na Vanessa wakiwa kwenye shoo jijini Mwanza katika ziara yao ya kimuziki mikoa mbalimbali waliyoipa jina la In love and Money Tour walionyesha mahaba jukwaani kwa kunyonyana ndimi hadharani ambapo picha yao ilikuwa gumzo kila kona baada ya kusambaa mitandaoni.

SIYO HAO TU

Tofauti na Vanessa na Jux hivi karibuni kumeibuka wimbi la wasanii wa muziki wawapo jukwaani wakifanya shoo kuonysha vitendo vilivyo kinyume na maadili akiwemo, Mbwana Kilungi ‘Mbosso’ ambaye aliitwa Basata na kuonywa na mwingine ni Lulu Euggen ‘Amber Lulu’ ambao wote wakiwa jukwaani walionyesha vitendo vya faragha visivyotakiwa kuonyeshwa hadharani

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.