The House of Favourite Newspapers

KAJALA, UWOYA, SANCHI… MGODI UMETEMA AU FIKSI?

MIAKA kadhaa nyuma, kuna staa mmoja (naomba nisimtaje jina lake) aliwahi kushambuliwa sana kutokana na tabia yake ya kupenda kuishi maisha ya anasa lakini nyuma ya pazia ikadaiwa kuwa, mbali na kupata mkwanja mrefu kupitia muziki, hakuwa na kitu chochote cha maana alichokifanya.

Yeye alikuwa ni mtu wa viwanja, ‘totoz’ kwa sana na kukodi magari ya kifahari huku akidai ni ya kwake. Huko kote ilikuwa ni kutaka kuwadanganya Watanzania kuwa, mambo yamemnyookea.

Baadaye ilipokuja kubumbuluka kuwa, yalikuwa ni maisha feki, aibu ilibaki kuwa kwake. Lakini, wakati staa huyo akibaki na aibu yake, zipo tambo nyingine za mastaa Bongo kuhusu kutumia mamilioni ya pesa kwenye mambo flaniflani na kuacha vingi viulizo.

 

IRENE UWOYA

Juzikati staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya alijinasibu kuwa, aliandaa pati kwa pesa yake mwenyewe na kuwachukua marafiki zake kwenda kula nao bata ndani ya boti huko kwenye Ufukwe wa Bahari ya Hindi. Akadai alitumia kama shilingi milioni 15 keshi kutoka kwenye pochi yake.

 

Watu wakahoji, Uwoya huyu na ugumu huu anawezaje kutenga milioni hizo kwa ajili ya bata la siku moja tu? Ni kwamba anazo nyingi, ameshasaidia sana wasiojiweza, amefanya mambo mengi ya maana hadi imebaki chenchi ya kutumbua? Hakika wengi hawajapata majibu ya maswali hayo.

KAJALA MASANJA

Achana na Uwoya, Kajala Masanja naye siku za hivi karibuni akatamba kuwa saa na bangili alizovaa ameteketeza shilingi milioni 16. Akajitetea kuwa, watu wasidhani anajikweza maana saa hiyo ina thamani kubwa kutokana na kuwa na mchanganyiko wa dhahabu na almasi. Wadau wakahoji, saa na bangili tu kwa milioni 16, na usawa huu? Miguno ikachukua nafasi huku wengine wakienda mbele zaidi na kusema ni mbwembwe tu za mastaa.

 

SANCHI

Mbali na hao, kuna huyu mwanadada Jane Ramoy ‘Sanchi’ ambaye umaarufu wake umetokana na figa yake matata. Naye siku kadhaa nyuma alisema kuwa, watu wanamsema kwamba, licha ya kujianika mtupu mtandaoni, hana lolote la maana analofanya. Akaamua kufunguka kuwa ana bonge la kiwanja alichonunua milioni 97 huko Bunju jijini Dar na siku si nyingi atashusha mjengo wa maana. Tambo za mastaa hao ni gumzo kwa sasa huko mtaani. Watu wanajiuliza; ni kwamba mgodi wa pesa umetema kwao au ni fiksi tu?

 

Wadau wanahoji hivyo kutokana na uhalisia wa maisha ya sasa. Mastaa wengi nidhamu ya pesa imechukua mkondo wake, hawatumii ovyo. Hata zile ‘bethidei’ za kufuru zilizokuwa zikifanyika miaka ile, sasa hivi hakuna. Wengine wameuza magari yao ya kifahari, wamenunua magari ya kawaida huku baadhi wakitumia Bajaj na bodaboda.

Wengine waliitwa mapedeshee kwa tabia yao ya kumwaga mapesa kwenye shoo mbalimbali lakini sasa hivi hata kwenye kumbi za starehe hawaendi. Vyuma vimekaza! Lakini wakati hao wakibadilika, tunawaona akiwa Uwoya, Kajala wakionesha kwamba, kwao pesa siyo tatizo, matanuzi kama kawa.

Swali, ni kwamba wao wana vyanzo vya mapato vya kueleweka, pesa inaingia tu hadi inamwagikia kiasi cha kuweza kufanyia mambo mengine ya ‘show off’? Au nyuma kuna wanaume wanawapa jeuri ya pesa? Je, ni fiksi tu, kwamba mamilioni wanayoyatamka kuwa wameyatumia kufanyia mambo flani ni maneno ya kujikweza?

 

Yote yanawezekana lakini mimi niseme tu kwamba, huu siyo wakati wa kujisifia kwa kutumia pesa nyingi kwenye mambo yasiyo ya msingi. Ni wakati wa kuongeza nidhamu katika kila shilingi tunayoipata. Kama kweli Sanchi kwa vurugu zake tu mtandaoni amemudu kununua kiwanja cha milioni 97, ni jambo la kumpongeza na pongezi zaidi zitakuja pale atapojenga na huo mjengo alioahidi.

 

Kajala kununua saa na bangili kwa shilingi milioni 16, si jambo baya lakini mimi naona ni kufuru isiyo na faida. Saa ya milioni 16 ili iweje? Anyway, ni yeye na maisha yake. Ila Uwoya ni vyema akajitathimini. Hizi siyo zama na kutumia milioni 15 kuwalisha na kuwanywesha watu, kwa kipato kipi cha kueleweka? Umeshawekeza kwenye nini ambavyo vitakuhakikishia kupata pesa kiasi kwamba mil.15 wala siyo ishu kwako? Mimi nafunga mdomo wangu!

Na Amran Kaima

Comments are closed.