The House of Favourite Newspapers

Kama Hujazungukwa Na Watu Sahihi, Mafanikio Utayasikia Tu!

NI wiki nyingine tunakutana tena kupitia safu hii nikiamini umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Mimi namshukuru Mungu kwa kunikutanisha nanyi tena kupitia ukurasa huu ambao unagusa maisha yetu kwa kiasi kikubwa.

 

Wiki hii msomaji wangu nataka kuwazungumzia baadhi ya watu ambao wao wapowapo tu, wameridhika na maisha yao duni lakini haohao ndiyo wako msitari wa mbele kuwakatisha tamaa wenzao wanaopambana kutimiza ndoto zao.

 

Ukweli ni kwamba, maisha ya sasa yana changamoto nyingi, wanaoweza kuishi kwa furaha ni wale ambao kila siku wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii, lengo likiwa ni kuyaboresha maisha yao pamoja na wale wanaowategemea.

Achilia mbali hao ambao wanapambana kuyaboresha maisha yao, wapo ambao wamekuwa wakiota kuwa na mafanikio makubwa sana.

 

Wamekuwa wakiumiza vichwa vyao juu ya nini wafanye ili mwisho wa siku ndoto zao ziweze kuwa kweli.

Hawa ni wale wanaojua maana halisi ya maisha. Wanajua mafanikio ni kwa kila mtu na kwamba anayeishi ili mradi siku zinakwenda, hawezi kuwa na faida yoyote kwenye jamii anayoishi.

Wenye mawazo hayo ndiyo wale ambao siku hadi siku huona mabadiliko katika maisha yao. Wanaaga umasikini kwa kasi. Mimi na wewe tunatakiwa kuwa hivyo. Kuamini kwamba maisha ya kuwa na uhakika wa kula, kulala na kuvaa tu siyo tuliyopangiwa.

 

Maisha sahihi tuliyopangiwa ni kuwa na uhakika wa kujipatia mahitaji hayo muhimu lakini pia kuwa na ziada ambayo itatufanya tuwasaidie wale ambao hawana uwezo.

Hapa nawazungumzia walemavu, watoto yatima na wazee. Hawa wanahitaji msaada wako, sasa kama utaridhika na maisha eti kwa kuwa umeweza kujikimu wewe na familia yako, utakuwa unakosea.

 

Lakini sasa wakati wewe na mimi tukiwa kwenye jitihada za kutimiza ndoto zetu, wapo watu ambao wanashangaza sana. Nawazungumzia wale ambao wamekuwa na tabia ya kuwakatisha tamaa wenzao wenye uchu wa mafanikio.

Watu hawa wapo huko mtaani. Unakuta wewe unakesha usiku na mchana, unapambana ili kutimiza ndoto zako, anatokea mtu kwa chuki zake anakuendea kwa mganga ili usifanikiwe au anakutia maneno ya kukuvunja moyo ili usitimize malengo yako.

 

Watu hawa ni wabaya sana na ni adui wakubwa wa mafanikio.

Inawezekana kabisa wewe huna shida ya kufanikiwa, umeridhika na maisha yako duni unayoishi, kwa nini sasa uwe kuzuizi kwa wengine wanaotaka kuzifanya ndoto zao ziwe kweli?

Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba, siku zote safari ya kuelekea kwenye mafanikio siyo ya lami, ina mashimo, milima na mabonde kiasi kwamba ili kufika kule unakotaka, inahitaji moyo na sapoti pia kutoka kwa watu wanaokuzunguka. Ukiwa umezungukwa na watu wenye wivu, chuki na husuda, kufanikiwa kwako itakuwa ni kazi sana, waepuke hao!

 

Ndiyo maana unashauriwa kuchagua marafiki, washauri sahihi ambao unaamini ukiwashirikisha kwenye mawazo yako, wanaweza kukuunga mkono na kukupa sapoti inayostahili badala ya kukuvunja moyo.

Pointi ya msingi leo ni kwamba, mimi na wewe tunatakiwa kuhakikisha ndoto zetu zinatimia. Kikubwa ni kuzishughulisha akili zetu na kuweka malengo kwa kupita kule walikopita wale waliofanikiwa kabla yetu.

Kingine ni kuhakikisha tunachagua watu sahihi wa kuwashirikisha mipango yetu ya kusaka mafanikio. Siyo kila mtu atakuunga mkono, wengine watakukatisha tamaa, hiyo chukulia ni changamoto.

 

wKatika hili la kuchagua watu sahihi wa kukufikisha kwenye ndoto zako, namaanisha marafiki na hata ndugu zako. Kumbuka si kila ndugu atafurahi kuona unafanikiwa, wengine watataka kukuona uko vilevile kila siku, yaani mfanane. Hao wagundue haraka na kuwa nao mbali.

 

Hata kwa wewe ambaye uko kazini, tambua kuna wafanyakazi wenzako watataka kukuona kila siku unakuja kwa miguu kazini. Ukiwaambia unataka kununua gari watakukatisha tamaa. Ukigusia suala la kujenga nyumba, wataonesha kuna ugumu katika hilo hasa kipindi hiki. Hao ni watu wabaya sana ambao hawataki kukuoa unabadilika. Wanataka maisha yako ya jana, leo na kesho yabaki vilevile, waepuke.

 

Mwisho nishauri tu kwamba, kama wewe huna tamaa ya kufanikiwa, waache wenzako wanaojua lengo la kuletwa hapa duniani watimize ndoto zao. Kama unajua huna uwezo wa kufanikiwa labda kutokana na sababu unazozijua, basi watie moyo wenzako kwani kufanikiwa kwao kunaweza kuwa na faida kwako.

Makala na Amrani Kaima Maoni/ushauri simu: +255 658 798787

Comments are closed.