The House of Favourite Newspapers
gunners X

Kifo cha Mzeew Mkapa ni Simanzi kwa Taifa

0

SIMANZI imetawala kila kona ndani na nje ya Tanzania kufuatia msiba mzito wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa.

Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa na umri wa miaka 81.

Rais Dk John Pombe Magufuli ametangaza kupitia runinga ya Taifa taarifa ya kufariki dunia kwa kiongozi huyo wa awamu ya tatu kilichotokea katika hospitali moja jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

“Mzee Benjamin William Mkapa Rais wa Awamu ya Tatu amefariki. Amefariki kwenye hospitali mjini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa.

“Niwaombe Watanzania tulipokee hili. Taifa limepata msiba mkubwa. Tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele ya haki,” ametangaza Rais Magufuli.

Taarifa hiyo, hata hivyo, haikuweka wazi Mzee Mkapa alikuwa akisumbuliwa na maradhi gani.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Mtandao wa Twitter, Rais Magufuli amemuombolezea Mkapa na kusema atamkumbuka;

“Kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi.”

Taarifa zaidi juu ya msiba huo na mipango ya mazishi zinatarajiwa kutolewa baadaye.

Mzee Mkapa alizaliwa Novemba, 1938 mkoani Mtwara Kusini mwa Tanzania na aliliongoza Taifa kwa mihula miwili tangu mwaka 1995 hadi 2005.

Kufuatia simanzi hiyo kubwa, Rais Magufuli ametangaza siku 7 za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo (Ijumaa ya Julai 24, 2020).

Amesema katika kipindi chote cha maombolezo, bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Kufuatia msiba huo mkubwa, watu mbalimbali wameeleza kushtushwa na habari za kifo cha Mkapa kuanzia viongozi, wanasiasa, wasomi, mastaa na watu wa kila kada.

Mara ya mwisho kuonekana kwenye shughuli za kiserikali iikuwa Mei 30, mwaka huu katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ambapo Rais Magufuli alimkabidhi zawadi ya ndege aina ya tausi 25 kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wastaafu.

WASIFU WA MKAPA

Benjamin William Mkapa amezaliwa Novemba 12, 1938. Alikuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu 1995 hadi 2005 na Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi -CCM (Revolutionary State Party).

Mkapa ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Makerere. Nafasi alizoshikilia zamani ni pamoja na kuwa Ofisa Utawala huko Dodoma na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Pia aliongoza ujumbe wa Tanzania nchini Marekani na alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje tangu 1977 hadi 1980 na kutoka 1984 hadi 1990.

Katika mwaka wa 1995, Mkapa alichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, msingi wake ulikuwa ni kampeni maarufu ya kupambana na ufisadi na kuuungwa mkono kwa nguvu na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Juhudi za Mkapa za kupambana na ufisadi ni pamoja na kuumba jukwaa la wazi lililoitwa Tume ya Rais juu ya Ufisadi (Tume ya Warioba) na kuongeza msaada kwa Ofisi ya Kuzuia Ufisadi.

Muhula wa pili wa miaka 5 wa Mkapa kama Rais uliisha Desemba 2005. Katika wakati wake ofisini, Mkapa alibinafsisha kampuni zilizomilikiwa na Serikali akaweka sera za soko huria.

Wafuasi wake walimtetea kuwa kuvutia uwekezaji wa kigeni ungesaidia kukuza uchumi. Sera zake zilipata msaada wa Benki ya Dunia na IMF na kusababisha baadhi ya madeni ya nje ya Tanzania kufutiliwa mbali.

Baada ya kumaliza muda wake wa urais kwa kukamilisha mihula miwili inayoruhusiwa, aliteuliwa katika Bodi ya Wadhamini ya Chuo cha Aga Khan mwezi Novemba 2007.

Ametumika katika shughuli za usuluhishi wa migogoro ya nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo Burundi.

Mkapa alitunukiwa tuzo za heshima zisizopungua kumi.

Kabla ya umauti kumfika aliandika vitabu mbalimbali, lakini cha hivi karibuni ni kile cha My Life My Purpose.

Mkapa ameacha mjane ambaye ni mama Anna Mkapa na watoto wawili.

KUTOKA KWA MHARIRI

Uongozi na wafanyakazi wote wa Global Group tunaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mzito wa Taifa letu. Poleni Watanzania wenzetu. –Mhariri.

Stori: Sifael Paul. Ijumaa

Leave A Reply