The House of Favourite Newspapers

KIJANA ASIMULIA SIKU ZAKE 335 ZA MATESO NA MACHOZI

HUJAFA hujaumbika! Ndivyo unavyoweza kusema, pindi unapomuona, dereva wa basi aliyefahamika kwa jina la Peter Mbwana (pichani), mkazi wa Machimbo- Buza jijini Dar, anayeteseka kitandani kwa takriban siku 335 sasa baada ya kupata ajali mbaya.

Mbwana alipata ajali hiyo Agosti 29, mwaka jana na tangu hapo, amekosa msaada wa kifedha hivyo kushindwa kugharamia matibabu yake na kujikuta akilia na familia yake iliyokata tamaa juu ya hatma yake.

 

Akizungumza na Uwazi akiwa nyumbani kwake, Mbwana ambaye amedai alikuwa dereva wa Kampuni ya Dar Express akifanya safari za Dar-Moshi, alisema alipata ajali hiyo alipokuwa anakwenda kituo cha mabasi Ubungo kwa ajili ya kupakia abiria kuelekea Moshi. “Nakumbuka siku hiyo nilidamka na kwenda kufuata gari yadi na kuelekea Kituo cha Mabasi Ubungo kupitia Barabara ya Mandela, nilipofika maeneo ya Buguruni niliwapakia wapiga debe wa Ubungo mara nyingi huwa tunawasaidiaga.

 

“Baada ya kuwapakia, nikawa naelekea Ubungo nilipofika maeneo ya Tabata-Relini, taa zilikuwa hazijaruhusu nikasimama. Baada ya dakika kadhaa, taa ziliporuhusu nikaendelea na safari, ghafla nilipovuka tu kwenye zile taa, nikakutana na gari la mafuta nadhani dereva wake alikuwa amefeli breki, nimekuja kuliona lile gari la mafuta limevuka ukingo wa barabara toka upande wa kwenda Buguruni likaja kugongana na basi nililokuwa naendesha mimi uso kwa uso,” alianza kusimulia kwa uchungu huku akiwa hoi kitandani kwake. Akizidi kusimulia tukio hilo, Mbwana alisema kitendo cha lori lile kumgonga uso kwa uso, basi lake liliharibika vibaya na yeye alirushwa kupitia kioo cha mbele.

 

“Kiukweli kwa upande wa basi nililokuwa naendesha liliumia sana, mimi nilirushwa mbele ya gari kupitia kioo cha mbele kwa kuwa kilipasuka, nikawa nasikia sauti kwa mbali zikisema tusaidieni tunakufa baada ya pale bahati nzuri askari walikuwepo pale wakatuchukua na kutupeleka Kituo cha Polisi cha Buguruni, tukatoka pale na ile gari ya polisi tukaelekea Hospitali ya Amana.

 

“Nakumbuka pale tuliwaacha baadhi ya majeruhi nahisi ni wale ambao niliokuwa nimewapa lifti mimi na mwingine mmoja tulipelekwa Muhimbili (Hospitali ya Taifa) baada ya pale dokta akawa amenipima na kukuta mguu wangu huu wa upande wa kushoto umevunjika mshipa mkubwa basi kukawa hamna jinsi alivyowaambia ndugu zangu ikabidi tukubaliane kama familia nikakatwa mguu na huu wa kushoto ulivunjika mara nane ikabidi niwekewe antena.

 

“Baada ya kukatwa mguu, nikakaa kwa muda mfupi kisha nikarejeshwa nyumbani. Lakini tangu nimerudi nyumbani hali imezidi kuwa mbaya kwani ule upande niliowekea antena, unatoa tu uchafu na sasa sina fedha hata za kuweza kurudi hospitali.

 

“Ndugu wamejitahidi kadiri ya uwezo wao lakini nao wameshindwa kuweza kunipeleka tena hospitali na kama unavyojua mimi ndiyo nilikuwa msaada katika familia yangu nipo mimi na mke wangu ambaye hana kazi pamoja na mtoto wetu mmoja. “Dokta ameniambia inahitajika shilingi milioni 2 ili niweze pia kupewa mguu wa bandia angalau niweze kutembea lakini hiyo hela sina.

 

“Sijui hata huu uchafu unavyonitoka kwenye mguu una madhara kiasi gani katika mwili wangu kwa kweli nimejikatia tamaa maana kama kuhangaika kwa watu nimeshajaribu lakini sijapata msaada wowote, mimi hapa sina namna nasubiria tu Mungu afanye maamuzi yake,” alisema kwa uchungu huku machozi yakimtoka.

Kutoa ni moyo na si utajiri, kwa yeyote ambaye ameguswa kumsaidia Mbwana anaweza kumtumia chochote kupitia namba 0716076602.

Stori: NEEMA ADRIAN, Dar

Comments are closed.