The House of Favourite Newspapers

KIKAPU DAR… KWA MIKAKATI HII MNASTAHILI PONGEZI

NIANZE kwa kutoa pongezi kwa uongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) kwa kufanikiwa kuendesha Ligi ya Mkoa huo (RBA) ndani ya mwaka huu wa 2019.

 

Pamoja na changamoto mbalimbali wanazopitia ikiwemo miundombinu lakini pia suala la wadhamini, BD imekuwa imara katika kuhakikisha mechi za ligi ya RBA zinachezwa ili malengo wanayokusudia yatimie.

 

Moja ya malengo ambayo BD wanayataka kupitia ligi hiyo inayoendelea na mzunguko wake wa pili, kumsaka bingwa upande wa wanaume na wanawake, atakayewakilisha mkoa wa Dar kwenye mashindano ya Taifa (NBL), mwakani.

Baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika, nakumbuka ilikuwa Juni 16 mwaka huu pale kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, BD iliruhusu timu zote ambazo ni 24 zikiwemo 16 za wanaume na zilizobaki ni wanawake, kujipanga na mzunguko wa pili kwa kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza ndani ya ngwe ya awali.

 

Ipo hivi, wiki moja iliyopita, viongozi wa BD na wadau wake walikutana faragha kuyajenga mambo kadha wa kadha yanayohusiana na ligi ya mkoa wa Dar, kuanzia hatua ya mzunguko wa pili hadi fainali. Huyu hapa Kamishna Ufundi na Mipango wa BD, Gosbert Boniface anaweka wazi, baada ya Championi kutaka kujua nini kilizungumzwa kwenye kikao chao kilichofanyika wiki mbili zilizopita.

 

VIINGILIO “Katika mkutano wa viongozi wa BD na klabu zote zinazoshiriki RBA, tulijadili na kukubaliana tuanze mchakato wa kutoza mashabiki viingilio katika mechi zetu zinazochezwa, lengo ni kuwajengea utamaduni wa kuchangia maendeleo ya kikapu kama ilivyo kwa nchi za wenzetu wakiwemo majirani Kenya na Uganda.

 

“Viingilio kwa wadau watakaokuwa wanahitaji kuangalia mechi za RBA vitaanza kutozwa kuanzia hatua ya robo fainali na gharama yake haitazidi shilingi elfu moja, fedha zitakazopatikana tutazitumia katika mahitaji muhimu kama vile kulipa walinzi watakaosimama milangoni lakini pia kuna watu wa usafi na hata waamuzi wanaochezesha mechi kila siku.

 

MDHAMINI MPYA “Pamoja na kwamba mdhamini wa kwanza (Pepsi) tunaendelea
kuzungumza naye bado tunambembeleza ili atusaidie walau vinywaji vya kila siku kwa wachezaji, yupo mwingine ambaye ni kampuni ya Azam aliyeahidi kurusha baadhi ya mechi za RBA.

 

“Azam tunatarajia kuwa nao ndani ya mzunguko wa pili na kuendelea, naamini ujio wao utaleta manufaa katika mchezo huu kupitia ligi ya RBA.

 

“Kwa upande wa Pepsi, wameahidi mengi mwishoni mwa ligi nikimaanisha zawadi kwa timu bingwa na wachezaji watakaotakata, pamoja na hayo yote bado sisi kama BD tunapambana kuhakikisha wadhamini watamiminika ili wadau wakiwemo wachezaji wanufaike,” anaeleza Gosbert.

 

ISHU YA VIWANJA VIPYA Kutokana na changamoto ya kuvuja kwa paa la Uwanja wa Ndani wa Taifa, Gosbert ameweka wazi kuwa katikati ya mwezi ujao wataambatana na Rais wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF), ili wakapige hodi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa viwanja vya kikapu ambavyo aliahidi kujenga.

 

“Lengo ni kutaka atekeleze ile ahadi yake aliyoiweka, kama ambavyo unajua kile cha ndani cha Taifa jukumu la kukiboresha ni la Serikali ambapo kila tukiwaambia wahusika wanasema tusubiri watakapopata fedha watatekeleza,” anaeleza.

 

USIKU WA TUZO “Moja ya jambo kubwa ambalo tunataka kulifanya na tulilijadili kwenye kikao na viongozi wa klabu zote zinazoshiriki RBA ni uwepo wa usiku wa tuzo baada ya fainali za mwaka huu.

 

“Uwepo wa tuzo hizo utaleta mapinduzi makubwa mno katika mchezo wa kikapu, ukizingatia haikuwahi kufanyika miaka mingi, mfano mzuri ni ule ambao Simba SC wametoka kufanyiwa na bosi wao Mohammed Dewji ‘MO’ baada ya kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/19.

 

“Katika usiku huo, tutawaalika watu mbalimbali wenye wadhifa wao lakini pia wachezaji wapate tuzo kulingana na viwango vyao, washangiliaji bora na hata waandishi ambao wamekuwa kipaumbele katika kuripoti ligi ya RBA mwanzo hadi mwisho.”

Comments are closed.