The House of Favourite Newspapers

KILICHOTOKEA MBELE YA MAKONDA, SHEHE MKUU AMLIPUA DIAMOND

DAR ES SALAAM: Kufuatia kilichojiri ukumbini usiku wa kuamkia juzi Jumatatu, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, amemlipua ‘live’ kwa mara nyingine mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Risasi Mchanganyiko lina habari kamili.

TUJIUNGE HYATT REGENCY HOTEL

Tukio hilo lilijiri kwenye Usiku wa Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Sunday Manara ambaye alizindua pafyumu yake ya De La Boss na Taasisi ya Haji Manara aliyoianzisha kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) katika kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa (birthday). Shughuli hiyo kubwa ilifanyika kwenye Ukumbi wa Hyatt Regency The Kilimanjaro Hotel, Posta jijini Dar na kuhudhuriwa na mastaa wengi akiwemo Diamond na mchumba’ke wa sasa, Tanasha Donna Oketch na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Miongoni mwa waalikwa alikuwemo Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

MAKONDA ASABABISHA

Alipopewa fursa ya kuzungumza, RC Makonda alimpongeza Manara kwa hatua hiyo kubwa kisha alimuita Diamond au Mondi na Tanasha mbele ya Shehe Alhad na kuwatishia kuwa angewafungisha ndoa ya mkeka, jambo ambalo alilifanya kwa utani na kusababisha ukumbi kulipuka kwa vicheko. Wakati Makonda akitamka hayo, wote, yaani Shehe Alhad, Diamond na Tanasha walikuwa wamesimama mbele ya ukumbi na hapo ndipo minong’ono ikaibuka. 

RISASI LADODOSA

Ilibidi Gazeti la Risasi Mchanganyiko kudodosa kujua kunani ukumbini humo na kubaini kwamba chanzo cha minong’ono hiyo kilikuwa ni Tanasha.Lilipotaka kujua Tanasha amefanyeje, baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislam walisema kuwa vazi la gauni la bluu alilovaa mwanadada huyo lilikuwa limemuacha wazi mno hasa kwenye maumbile yake nyeti ya kifuani (matiti) na upaja kutokana na mpasuo wa nguo hiyo.

 

“Jamani…jamani…ndiyo nguo gani ile mbele ya kiongozi wa dini? Kiukweli si sawa na ndiyo maana hata Shehe Alhad alikataa kumpa mkono Tanasha na kuishia kumpungia. “Kwani Tanasha hakujua au hakuambiwa anakwenda kwenye mkusanyiko wa watu wengi wa kada mbalimbali ili ajisitiri? Ona sasa anavyoaibika hata anashindwa kutazama watu kutokana na aibu.

 

“Lakini yote kwa yote, wa kulaumiwa hapa ni Diamond kwani ndiye aliyetakiwa kumpanga mtu wake juu ya namna ya kuvaa kwenye shughuli kama hii. Kiukweli atakuwa amemtibua mno Shehe Alhad,” alisema mmoja wa wahudhuriaji waliokuwa wamedamshi ile mbaya.

 

SHEHE MKUU NA RISASI

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko juu ya kitendo hicho na kwamba alikichukuliaje, Shehe Alhad alitema nyongo kwa kumvaa Mondi mzimamzima. “Diamond hakufanya kitu kizuri, lakini alitekeleza amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar (Paul Makonda) kujitokeza pale mbele na mwenzake (Tanasha).

 

“Lakini hata mimi nilivyokwenda pale mbele sikupendezwa kumuona huyo mwanamke na ndiyo maana hata hukuniona nikimpa mkono wangu. “Ila niliheshimu kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar kwa kumpa mkono Diamond, lakini yeye (Tanasha) sikumpa mkono kwa kuwa nilimuona yupo vile.

DIAMOND DHAIFU

“Lakini pia Diamond naye anaonesha udhaifu kwa mwanamke kwa kumuacha namna ile kwa sababu mali zako lazima uzione wewe mwenyewe, mwanaume lazima uwe na wivu, haiwezekani unayetarajia kumuoa mwili wake unakuwa wazi ina maana hana thamani. “Diamond anatakiwa kumuongoza yule binti (Tanasha), hakutakiwa kumuacha vile.

 

“Unapomuacha vile bidhaa inaonekana na kila mtu ina maana haina thamani, huwezi kukuta dhahabu Kariakoo-Sokoni au Buguruni-Sokoni imeachwa, utakuta tu nyanya na vitunguu, hii ina maana kitu chenye thamani hakionekani ovyo, kwa hiyo Diamond ameonesha udhaifu na mimi sikupenda na mkono wangu sikuutoa,” alifunguka Shehe Mkuu Alhad huku akisisitiza kuwa hakupendezwa na muonekano wa Tanasha ambaye ni mke mtarajiwa wa Mondi.

SI MARA YA KWANZA

Mara kadhaa Shehe Alhad amekuwa akimshukia Mondi kwa ishu mbalimbali hasa suala la kusali, kufunga ndoa na kutojionesha kuwa ana mali nyingi mbele za watu.

Comments are closed.