The House of Favourite Newspapers

Kisa Fumanizi; Imamu wa Msikiti Yamkuta

IMAMU Msaidizi wa Msikiti wa Mahalai, uliopo katika Kijiji cha Mhalaka, Kitongoji cha Kipungili, Kata ya Doma, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Fadhil Mohamed yamemkuta ya aina yake baada ya kutelekezewa watoto wawili na mkewe, Nasra Abdallah kisha kujikuta kwenye wakati mgumu kwani mmoja kati ya watoto hao ni mdogo anayehitaji kunyonya maziwa ya mama.

 

Imeelezwa kuwa, chanzo cha tukio hilo lililotokea hivi karibuni ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani (unaotarajiwa kuwa Mei 16 au 17, kutegemea na mwandamo wa mwezi), ni baada ya mke wa imamu huyo, kudaiwa kufumaniwa na majirani zake akiwa na mchepuko wakati mumewe alipokuwa kwenye ibada.

Imedaiwa kuwa, baada ya kufumaniwa, ndipo Nasra alipoona isiwe tabu, akaamua kutokomea kusikojulikana na kumuachia mumewe huyo watoto hao wawili akiwemo huyo mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Baada ya Kamanda wa Kikosi Maalum cha Oparesheni Vichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kupewa mchapo huo, alitinga kijijini hapo na kuzungumza ana kwa ana na imamu huyo.

 

“Mimi ni imamu msaidizi wa msikiti huu, ninaishi hapa kwenye nyumba ya msikiti na familia yangu.

“Cha ajabu, siku hiyo (lilipotokea tukio) wakati ninaswalisha, mke wangu alitoweka nyumbani na kuniachia watoto wetu wawili, Rakibu mwenye umri wa miaka mitano na Aisha wa mwaka mmoja na nusu ambaye bado alikuwa ananyonya.

“Chanzo cha kuondoka sikijui, lakini nilielezwa kuna uovu aliufanya hivyo kwa aibu, aliamua kukimbia hapa kijijini na kutimkia Dar,” alisema imamu huyo.

Akizidi kusimulia, imamu huyo alisema baada ya mkewe kutoweka, mtoto mchanga alianza kumsumbua kwa kutaka ziwa la mama yake, akalazimika kumpeleka nyumbani kwao Ifakara.

“Baada ya mtoto mchanga kulia sana, kila siku nyakati za usiku akitaka joto na ziwa la mama yake, niliamua kumpeleka nyumbani kwetu, lfakara.

“Baadaye niliambiwa kuwa mke wangu katorokea Dar, nilifanikiwa kumkamata jijini humo ambapo alisafirishwa na kulala Kituo cha Polisi cha Morogoro Mjini na baadaye aliletwa hapa Doma, akalala tena rumande kasha akatoka kwa dhamana.

 

“Tuliitwa nyumbani lfakara kwa mazungumzo ya kifamilia ambapo kwenye kikao hicho niliziomba familia zote, yaani ya kwangu na ya mke wangu wanipe muda kwanza nitafakari jambo hili,” alisema imamu huyo.

Alipoulizwa kama ana mpango wa kurudiana na mkewe huyo, alijibu: “Niliongea naye, akasema nikitaka kurudiana naye, kutokana na aibu aliyoipata, itabidi tuhame kijiji hiki na mimi kituo changu cha kazi ni hapa msikitini hivyo nilishindwa kukubali kurudiana naye kwa sharti hilo.”

 

Alipobanwa zaidi kuhusiana na mkewe huyo kufumaniwa wakati yeye akiwa msikitini akiswalisha, imamu huyo alisimulia:

“Ni kweli, hata mimi taarifa hizo za mke wangu kufumaniwa na watu akiwa na mwanaume mwingine wakati mimi nikiwa msikitini nimezisikia.

“Lakini baada ya kufanya uchunguzi, sikuweza kuthibitisha hivyo dini yetu (Uislamu) inataka kumhukumu mtu kwa uthibitisho na si maneno ya kusikia ndiyo maana nilimtaka mke wangu arudi, lakini kwa aibu hiyo aligoma kurudi hapa kijijini.”

 

MAZINGIRA YA TUKIO

Habari zilizozagaa kijijini hapo zilidai kwamba, mke huyo wa imamu alikuwa na tabia ya kuchepuka kwa kutumia mwanya wa mumewe kuwa msikitini akiongoza ibada na ndipo 40 yake ilipofika hivi karibuni.

Mtoa ubuyu mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Saidi, mkazi wa eneo hilo alieleza namna ambavyo ilikuwa rahisi kwa mke huyo wa imamu kubainika uovu wake kirahisi:

 

“Kama unavyoona kijiji chetu ni kidogo hivyo kila mara imamu akiwa msikitini, mkewe alikuwa anatoka na kwenda kwenye nyumba ya jamaa yake na kujifungia ndani.

“Sasa siku hiyo watu wakakosa uvumilivu walipomuona akitoka kwenye nyumba ya jamaa huyo asiye na mke, majira ya saa 7:00 mchana, akiwa amevaa juba (koti kubwa lenye ukosi na mikono mipana linalofanana na joho), walimvaa na kumhoji.

 

“Badala ya kujibu, mke huyo aliparamia bodaboda na kukimbia na kumuachia mumewe watoto wawili,” alisema shuhuda huyo.

Ijumaa Wikienda lilijaribu kumvutia waya mke huyo wa imamu lakini simu yake haikupatikana hewani. Jitihada za kumtafuta zinaendelea.

Stori: Dunstan Shekidele, Moro.

BARNABA: Hii Siyo Sababu Iliyopelekea Kuachana na Mama Steve

Comments are closed.