The House of Favourite Newspapers

Kisa mabilioni ya GSM, Mo Aanza Kufuru

0

BILIONEA wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameanza kufuru mpya na safari hii ameanza na jaribio la matajiri wa Yanga Kampuni ya GSM iliyomtengea mamilioni kiungo wake Hassani Dilunga ili kuhakikisha anatua Jangwani.

 

GSM hivi karibuni ilielezwa kuwepo kwenye mipango ya kumpeleka kiungo huyo Jangwani kwa dau la Sh Mil 80 alizowekewa mezani.

 

Kiungo huyo ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu, wengine ni Mzamiru Yassin, Sharraf Eldin Shiboub, Yusuph Mlipili, Pascal Wawa na Deo Kanda ambaye naye yupo kwenye mipango ya usajili Yanga.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu, imezipa kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, mwekezaji wa klabu hiyo ambaye ni bilionea Mo hatakubali kumuachia mchezaji yeyote muhimu na tegemeo Simba.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa tayari bilionea huyo ameanza kufanya mazungumzo na wachezaji wote ambao wamemaliza mikataba huku akiwaahidi kuwapa dau zito kila mmoja lile analolitaka ili mastaa hao wasitue Yanga.

 

Aliongeza kuwa bilionea huyo amepanga kuwabakisha kutokana na wachezaji hao wote kuwepo kwenye mapendekezo ya ripoti ya kocha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck aliyoikabidhi kwenye Kamati ya Usajili ya timu hiyo.

 

“Mo hatakubali kumuachia Dilunga aende Yanga, kwani tayari amepata taarifa za yeye kuwaniwa huko, ikiwatumia GSM kufanikisha usajili wake. “Hivyo amepanga kuanza na Dilunga ili kuzuia jaribio la GSM walio kwenye mipango hiyo.

 

“Baada ya kumalizana na Dilunga atahamia kwa Kanda, kisha atawarudia Wawa na Shiboub.

 

“Mo anajiamini katika hilo kwani ana uwezo wa kumpa dau zito la usajili Dilunga zaidi ya hilo alilowekewa na GSM ambalo ni Sh mil 80,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Dilunga kuzungumzia hilo alisema: “Yupo kwenye mazungumzo mazuri na uongozi wa Simba na kama mambo yakienda vizuri, basi nitaendelea kubakia Simba.”

 

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara hivi karibuni alitoa angalizo kwa viongozi na mashabiki wa timu hiyo juu ya ujio wa GSM.

 

“Lipo wazi ujio wa GSM una kishindo kikubwa na hilo lipo wazi utaona usajili bora walioufanya dirisha dogo umewafanya Yanga kuwa bora.

 

“Yanga walikuwa wana miaka mitatu hawajatufunga, lakini msimu huu wametufunga bao 1-0 na kutoka nao sare mabao 2-2, hiyo inamaanisha GSM wapo vizuri,” alisema Manara.

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply