The House of Favourite Newspapers

Kisa Mazembe, Kagere auwasha moto Simba

Meddie Kagere

MSHAMBULIAJI wa Simba raia wa Rwanda, Meddie Kagere, ameweka wazi kile alichoiandalia timu ya TP Mazembe katika mchezo wa kesho wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Simba itapambana na TP Mazembe kesho Jumamosi kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ambapo kila timu itakuwa ikihitaji ushindi ili iweze kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

 

Wakala wa Kagere, Patrick Gakumba ameliambia Championi Ijumaa kuwa, mteja wake huyo amemwambia kuwa katika mchezo huo wa kesho atapambana kufa na kupona ili aweze kuiongoza Simba kuibuka na ushindi. Alisema kuwa katika mchezo huo, Kagere amemwambia kuwa iwe kufa au kupona atahakikisha anapambana vilivyo mpaka awafunge TP Mazembe.

 

“Jana (juzi) nimezungumza na Kagere nikitaka kujua jinsi alivyojipanga kwa ajili ya mechi ya TP Mazembe na ameniambia kuwa yupo vizuri na atahakikisha anapambana kwa nguvu zake zote ili aweze kuifunga timu hiyo.

 

“Baada ya kuniambia hivyo na mimi nimemtaka ahakikishe anafanya hivyo kwa sababu thamani yake itaongezeka hata kile kitita cha dola 300,000 (zaidi ya Sh 700 milioni) ambacho hivi karibuni walimtangazia ili waweze kumsajili kinaweza kuongezeka.

 

“Kwa hivyo, niwaombe tu Wanasimba wajitokeze kwa wingi katika mchezo huo ili kuisapoti timu yao kama ambavyo wamekuwa wakifanya siku zote katika uwanja wao wa nyumbani tangu walipoanza michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu,” alisema Gakumba.

Stori na SweetbertLukonge

Comments are closed.