The House of Favourite Newspapers

Kisa Simba, Kocha wa Thomas Ulimwengu Atimuliwa

KUMEKUCHA Afrika! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Simba kuzua balaa nchini Algeria katika Klabu ya JS Saoura.

Simba iliichapa timu hiyo mabao 3-0 katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na taarifa mpya ni kwamba matokeo hayo yamesababisha kocha wa JS Saoura anayoichezea Mtanzania, Thomas Ulimwengu afukuzwe kazi.

 

Kipigo hicho pamoja na matokeo ya sare ya bao 1-1 ambayo JS Saoura iliyapata juzi Ijumaa ilipocheza na Al Ahly ya Misri, yamesababisha kocha mkuu wa timu hiyo, Nabil Neghiz atimuliwe.

Neghiz ametimuliwa kuifundisha timu hiyo baada ya uongozi wa klabu hiyo kutoridhishwa na matokeo ambayo Saoura imeyapata katika mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

 

Inadaiwa kuwa uongozi wa timu hiyo haukufurahishwa kabisa na matokeo hayo na ndipo ukachukua uamuzi huo wa kumtimua kocha huyo, kwani unaamini kuwa timu yao ipo vizuri na ilipaswa kuwa juu katika kundi lake la D.

Kwa sasa, JS Saoura katika Kundi D kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ndiyo inayoburuza mkia ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili.

 

Inayoongoza kundi hilo ni Al Ahly ya Misri ambayo ina pointi nne, nafasi ya pili inaenda kwa AS Vita yenye pointi tatu sawa na Simba lakini yenyewe ipo juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

AS Vita inayofundishwa na kocha Martin Ibenge, inaonekana iko vizuri na inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na kujaza wachezaji wengi mafundi na wenye nguvu.

Kocha wa Al Ahly, Martin Larsate raia wa Uruguay, naye atataka kupata matokeo bora dhidi ya Simba ili asiingie kwenye presha ya kutimuliwa.

 WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.