ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship Church, Zachary Kakobe amesema siku hizi baadhi ya wachungaji na manabii wanashangaza kutokana na tabia zisizo za kawaida wanazozifanya mbele ya madhahabu ikiwa ni pamoja kuwataka wanawake wasionasa ujauzito kuvua nguo zao za ndani ili wawaombee.
Akizungumza mbele ya mwandishi wetu baada ya mahubiri katika Jukwaa la Kumtangaza Kristo (JKK) katika kanisa la BCIC Mbezi jijini Dar hivi karibuni, Askofu Kakobe alisema siku hizi kuna manabii wanafanya mambo ya ajabu sana ambayo ukihadithiwa huwezi kuamini.
“Kuna manabii wanawaamuru wanawake kuvua nguo zao za ndani kisha huyo anayejiita nabii anaishika na kuiombea eti ili mwanamke huyo aweze kushika mimba na kwa kuwa watu wana shida, wanafanya hivyo, hili ni jambo baya kabisa,” alisema Askofu Kakobe huku akionyesha uso wa masikitiko na kuongeza:
“Acha hilo la wanawake kuvua nguo zao kanisani ili waombewe, zamani kulikuwa na mnajimu maarufu hapa nchini (Shehe Yahya Hussein), angekuwepo leo hapa angesema kwa nini wachungaji mnaniingilia katika utaalamu wangu? Ni kwamba kwa sababu hayupo, shughuli ya utabiri wa nyota inaingia kanisani?”
Kiongozi huyo wa kiroho alikemea ushetani huo mzito huku akitoa ushuhuda wa jinsi yeye alivyookoka. Alisema yeye alikuwa mwanamuziki wa dansi na alikuwa na studio ya kurekodi nyimbo za muziki Temeke na alikuwa na pesa lakini aliacha na kuokoka baada ya Askofu Moses Kulola kuhubiri, naye kumpokea Yesu.
Alisema tarehe sita mwezi wa nne, 1980 wakati anasubiri mabasi kwenda Moshi, aliona matangazo ya Askofu Kulola kwamba atahubiri Kariakoo, akaamua kwenda kumsikiliza kabla ya kusafiri kwa kuwa mabasi wakati ule yalikuwa yakisafiri usiku.
Alipokwenda kwenye mahubiri, injili ilimuingia na kuamua kuokoka.
“Siku moja nilikwenda kwenye muziki wa Juwata Jazz, nikaingia kwenye muziki, sauti ikanijia na kuniuliza, umekuja kufanya nini hapa na wewe umeokoka? Nikatoka ukumbini, getini mlinzi akaniuliza unatoka? Hutarudishiwa kiingilio chako; nikamjibu; potelea mbali na tangu siku hiyo nikaachana na muziki wa dansi,” alisema Kakobe.
Alisema leo kuna watu wameokoka kwa kusema Bwana Asifiwe lakini maisha yao ni yaleyale na ndio maana Yesu ameshuka ili kanisa lake liwe safi.
“Mtu akizaliwa katika Kristo, kila pombe inaondoka, sigara inatoka, uzinzi unatoka, kuokoka ni kubadilishwa maisha,” alisisitiza Askofu Kakobe.
Jukwaa la Kumhubiri Kristo (JKK) linaundwa na Askofu Kakobe, Askofu Sylivester Gamanywa na Apostle Vernon Fernandes, lengo likiwa kurudi katika kuhubiri jina la Yesu na kuachana na mambo ya mafuta ya upako, kuabudu nyota, chumvi, vitambaa na kadhalika kama zinaleta miujiza.
Askofu Kakobe alisema Wakristo wasipokuwa makini ya vitu hivyo, watajikuta wakiingia katika imani potofu ambayo haitawafikisha kwa Mungu.
Naye Askofu Sylvester Gamanywa aliungana na Kakobe na kusema wanao wajibu wa kukemea wachungaji au manabii wanaopotosha watu.
Alisema wao hawawasemi Wakristo isipokuwa wao wanamhubiri Kristo na hawapaswi kuomba kibali kwa yeyote.
Alisema Yesu Kristo alikataza watu kutoza waumini fedha kama wafanyavyo baadhi ya wachungaji na manabii ambao hutoza watu fedha au kuwauzia maji na mafuta.
“JKK tunapinga mambo yote yanayopotosha Ukristo, biashara isiyo halali ya kuuza mafuta na maji kwenye huduma ya maombezi kwa kisingizio cha ufunuo wa kinabii,” alisema Askofu Gamanywa na akasema katika vitabu vya Mungu hakuna mahali pameandikwa kuwa zana za upako ziliuzwa.
“Sisi tunachokipinga ni kile Kristo Yesu alikataa na ndio maana sisi JKK tunakataa na kazi yetu ni kutofautisha injili ya Kristo na injili nyingine,” alisema.
ASKOFU MWAMALANGA: NI UJAMBAZI
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashehe ya Maadili na Haki za Binadamu, Askofu William Mwamalanga alisema matukio hayo ni ujambazi sawa na ulivyo ujambazi mwingine kwa sababu wachungaji hao wanawalaghai na kuwadhalilisha wanawake.
“Ni ujambazi wa roho za watu na maisha yao, kumwambia mtu mambo ambayo si ya kweli kwa kutumia neno la Mungu ni hatari sana, kwa sababu wanawafanyia hivi kwa udanganyifu ili wawape fedha na kwa Tanzania mikoa iliyoathirika sana ni miji mikubwa mikubwa kama Dar, Mbeya, Mwanza na Arusha,” alisema.
Aidha, aliwaomba Watanzania kuwakataa wachungaji wa aina hiyo kwa kuwa hayo si mafundisho bali ni zaidi ya uchawi kama uchawi mwingine.
“Kumuombea mwanamke kwa kushika sehemu nyeti za mwanamke au mwanaume ni uongo, au kumuombea kuwa utapata malori au kwenda ulaya ni uongo. Hakuna Mungu anayefanya vitu hivyo.
“Hao watu hawajui madhara yake, wanaitwa manabii wa uongo, ila kesho ipo ambapo haya mambo yao ya uongo watakuja kulia vibaya,” alisema.
Hata hivyo alisema kamati hiyo inatarajia kuzungumza na vyombo vya dola ili kuwaainisha wachungaji wa aina hiyo na baadaye wafikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya udhalilishaji wa wanawake.
Upepo wa kisulisuli na ndoa
Hayo yanajiri katika kipindi hiki ambacho baadhi ya wachungaji katika makanisa mbalimbali nchini wanajaza waumini hasa wanawake kutokana kufuata mamombi ili wapate wanaume wa kuwaoa na kunasa mimba.
Aidha wiki iliyopita moja ya video iliyomuonesha Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Mlima wa Moto, Dk Getrude Rwakatare akiwaita madhabahuni wanawake na wasichana ambao hawajaolewa ili awafanyie maombi na watawapata wenza wao kwa “upepo wa kisulisuli, ilizua gumzo na kudhihirisha namna tatizo hilo linavyozidi kukua kila siku.
Pia ikumbukwe kuwa katika utafiti wa kufuatilia kaya Tanzania (National Panel Survey) wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ulionesha kuwa kiwango cha watu wasiooa au kuolewa kinazidi kuongezeka na kufikia asilimia 38.3 wakati waliomo kwenye ndoa wakiwa ni asilimia 34.8.
STORI: ELVAN STAMBULI


Comments are closed.