KITABU Cha Rais Mstaafu Mwinyi Chazinduliwa

Taasisi ya Uongozi Institute imesema rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ameagiza fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya kitabu cha maisha yake cha ‘Safari Yangu, Mzee Rukhsa’ zitumike kuandaa vitabu vya viongozi wengine.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Mei 8, 2021 na ofisa mtendaji mkuu wa taasisi hiyo, Kadari Singo katika uzinduzi wa kitabu hicho jijini Dar es Salaam, shughuli iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kitabu hiki kiliandikwa mwaka 2017 na kukamilika mwishoni mwa mwaka 2020…, na Rais Mwinyi amesema kuwa hatochukua hela yoyote itakayotokana na mauzo ya kitabu hiki, amesema fedha zipelekwe katika kuandaa vitabu vya viongozi wengine,” amesema Singo.
Amesema walipewa jukumu la kuongoza kada ya uongozi nchini, moja ya jukumu lake ni kuandaa tawasifu za viongozi.
“Kuzindua tawasifu ya Mwinyi ni mwendelezo wa jukumu la mradi za kuhifadhi taarifa za kumbukumbu za uongozi unaofanywa na taasisi hii. Itakumbukwa mwaka 2019 tulikutana hapa kuzindua kitabu cha Hayati Benjamin Mkapa,” amesema.
Ameongeza kuwa kuandika vitabu kuhusu maisha ya viongozi inasaidia wengi kujifunza namna bora ya kuishi, akibainisha kuwa viongozi wengi hawaandiki vitabu kutokana na kukabiliwa na mambo mengi.
“Haikuwa kazi rahisi kwa Rais Mwinyi kukubali uandishi wa kitabu hiki, na hii ni kutokana na kuwa anajua ugumu wa uandishi ulivyo. Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha fasaha ya Kiswahili na ameanisha sababu za kutumia lugha hiyo na inatoa sababu za kuunga juhudi za kukitangaza Kiswahili,” amesema.
Amebainisha kuwa, kimegharimu fedha nyingi, hasa katika uhakiki na usafirishaji ambapo kitauzwa na kupatikana katika maduka mbalimbali ikiwemo Mkuki na Nyota.

