The House of Favourite Newspapers

KUNA VIUMBE WA AJABU WANAOISHI ANGANI -3


NILIPOISHIA IJUMAA ILIYOPITA…
Nakumbusha kuwa katika uumbaji Mungu aliumba vitu vinavyoonekana na visivyoonekana. Wiki kadhaa niliona ni vyema tukajifunza vitu nje ya boksi. Ni juu ya uwepo wa viumbe wa ajabu waishi angani waitwao aliens. Kwa muda mrefu viumbe hawa wamekuwa wakiuhusishwa na upotevu wa vitu na watu duniani.

 

Wiki iliyopita niliishia pale tulipokuwa tunaangalia ukweli juu madai ya kuwepo kwa uhusiano kati ya wanasayansi wa Kimarekani na hawa Aliens ikielezwa kuwa wamekuwa wakibadilishana teknolojia. Je, hilo linawezekana? SHUKA NAYO…

 

Inaweza kukushtua kidogo, lakini baadhi ya watu wanaamini kuwa inapotokea Aliens wakapata ajali angani huwa Serikali ya Marekani inaagiza miili yao ifuatwe zaidi ya kilomita 1,448 kutoka eneo la Area 51 huko Las Vegas, Marekani ili kuwatibu majeraha. Eneo hili limekuwa maarufu mno kwa habari za Aliens na mauzauza yake. Baadhi ya watu husema Aliens wana maghala na stoo za teknolojia katika eneo la Area 51, wakishirikiana kwa karibu na wataalam wa anga wa Marekani.

 

Japo ni siri kubwa, lakini inaaminika kuwa wapo Aliens wanaoishi eneo hilo. Maswali juu ya hilo ni mengi hasa njia ya mawasiliano wanayotumia. Katika eneo hili mambo mengi ya kiteknolojia yamekuwa yakishuhudiwa na watu waishio jirani na eneo hilo. Kuna majengo ya ajabu ambayo ndani yake haijulikani kuna nini. Inaaminika hapo ndipo Aliens hubadilishana teknolojia na Wamarekani.

 

 

Kivipi? Wapo wanaoamini kuwa Aliens ndiyo huwaongoza wanasayansi hao hasa wanapokuwa kwenye jambo au jaribio la uvumbuzi wa teknolojia mpya. Inasemekana kwa sasa wapo kwenye mpango kujaribu kutengeneza kiumbe chenye mchanganyiko wa binadamu na Aliens kwa sababu hawawezi kuzaliana wenyewe.

 

Pia wamekuwa wakihangaika kuvumbua teknolojia ya uwezekano wa binadamu kuwasiliana na ndugu au jamaa ambao walishafariki dunia. Kuna madai kuwa serikali ya Marekani imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwekeza katika uvumbuzi huo huku binadamu wakitolewa wachinjwe bure ili kufanikisha jaribio hilo.

 

Wataalam wa anga wamekuwa wakikataa katakata kuwepo kwa uhusiano kati ya Aliens na Area 51. Pamoja na wataalam wa anga na marubani kukana habari hizo lakini bado wananadharia wa kisasa wameendelea kujenga dhana kuwa eneo la Area 51 lina uhusiano mkubwa na hawa Aliens.

 

Mwaka 1987, jamaa aitwaye Robert Lazar aliituhumu Serikali moja kwa moja kuwa ilikuwa ikishikilia aliens tisa katika eneo hilo ambao walikuwa wakisaidia kupatikana kwa teknolojia ya kuboresha masuala ya kivita angani. Kwa mujibu wa Lazar, aligundua uwepo wa mabaki ya vitu maalum alivyoviita Element 115 ambavyo vinafanana na hawa Aliens.

 

Watu wengi wanaamini madai ya Lazar ni ya uongo, lakini alipojitokeza kwenye televisheni mwanzoni mwa miaka ya 80 akifafanua mambo hayo, ndipo umma ukavutiwa na mawazo yake kuhusu hawa Aliens kwenye eneo la Area 51. Kwa miaka mingi sasa, Serikali imekuwa ikilitumia eneo hilo kujaribia ndege zake hasa za kivita na watu wengi wamekuwa wakiripoti kuona vitu visivyojulikana angani yaani UFO.

 

Juu ya UFO, wataalam wanadai kuwa watu wamekuwa wakipotoshwa na inawezekana wakaona ndege za kivita za kutisha tofauti na hizi za kawaida hivyo wakadhani ni UFO. Bado tumejikita kwenye eneo hili la Area 51. Tunatazama mauzauza yanayotokea eneo hili yakihusisha Aliens na wanasayanasi wa Marekani. Je, kuna uvumbuzi wowote uliofanikiwa? Usikose wiki ijayo.
Kwa maoni: 0713 750 910

Comments are closed.