The House of Favourite Newspapers

Lema Afunguka Kinachomuumiza Katika Siasa

0
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameweka wazi matatizo anayoyapata kama mbunge wa wananchi wake anaowatumikia, na kusema kwamba kama kiongozi wa wananchi,  huwa anauma sana moyoni anapoona wananchi hao hawaelewi wanachokifanya viongozi wao.

 

Lema ameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara kwenye kampeni  ya chaguzi mdogo ya udiwani katika kata ya Muriet mkoani Arusha, na kueleza kwamba wao kama wabunge  wanajitoa mhanga kuwatetea wananchi wao, lakini huwa wanaumia zaidi pale wananchi hao wanapooonekana hawajali wala hawaoni jitihada zao.

 

“Mimi ni mbunge ambaye nimekaa hospitali kumuuguza mbunge mwenzangu ambaye amepigwa risasi. Tundu Lissu amepigwa risasi kwa sababu ya kutetea uhuru wenu, tukiona hamuelewi mnatuumiza kuliko hao wanaotupiga, kama kuna  mateso tunapata kama viongozi wenu  na nyie ambao tunawapigania hamtuelewi, tunaumia kuliko maelezo”, amesema Godbless Lema.

Ameendelea kusema kwamba yeye binafsi anakumbana na changamoto nyingi kwani tangu apate wadhifa huo hajawahi kupata raha, kutokana na misukosuko anayoipata kutoka  jeshi la polisi  ambalo limekuwa likimdhalilisha.

 

“Toka nimekuwa mbunge wenu sijawahi kupata raha katika uongozi wangu, mimi ni mbunge ambaye nimepigwa sana, nimedhalilishwa sana na polisi.  Ni mbunge ambaye nyumbani kwangu polisi wamesachi mpaka nguo za ndani za mke wangu, kunidhalilisha na kunitisha.  Nimekwenda jela miezi minne na siku kumi na mbili, nimetekwa ili kuuawa, nimefukuzwa bungeni, kesi nilizonazo ni nyingi, nina kesi mbili dhidi ya rais na siogopi, na haya yote kwa ajili yenu nyinyi,” amesema.

Ameongeza kwamba amekuwa mbunge ambaye mara kwa mara anakabiliana na jeshi la polisi kwa makosa mbalimbali anayotuhumiwa, ambapo mpaka sasa bado ana kesi zinazomkabili mahakamani.

Leave A Reply