The House of Favourite Newspapers

Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Premium Lite kuzinduliwa leo

 

LIGI Kuu ya Wanawake inayodhaminiwa na Serengeti Premium Lite inatarajiwa kuzinduliwa leo Jumamosi kwa mchezo mmoja kupigwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar.

 

Mchezo huo unaotarajiwa kuwa na upinzani utakuwa baina ya wenyeji Evergreen dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, JKT Queens saa 10 jioni.

 

Mechi zingine za ligi hiyo ambayo inashirikisha timu 12 zitapigwa kesho Jumapili kwenye viwanja mbalimbali.

 

Akizungumza kuelekea kwenye uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Serengeti Premium Lite, Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Wanawake, Amina Karuma amesema msimu huu utakuwa na ushindani mkubwa.

 

“Ni ukweli usiopingika kwamba ligi yetu ya wanawake ambayo inadhaminiwa na Serengeti Premium Lite inaongezeka chachu ya ushindani na tunatarajia msimu unaoanza utakua na ushindani zaidi,” amesema Karuma.

 

Naye Ofisa Masoko wa Serengeti Breweries, George Mango amesema: “Serengeti Breweries Limited kupitia kinywaji chake cha Serengeti Premium Lite imewekeza kiasi cha Shilingi milioni 450 ili kuwezesha ligi hii ya wanawake iwe ya ushindani mkubwa na kuwaletea msisimko mashabiki wa soka hapa nchini.

 

“Watanzania wakae tayari sasa kuona burudani maridhawa kutoka kwa timu zinazoshiriki ligi hii. Hakika ni ligi inayotarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu sana. Tumeona namna ambavyo ligi ilivyoweza kutoa misisimko na msimu huu timu zimeongezeka kutoka 8 kwenye ligi mwaka jana hadi 12 za sasa.”

 

Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni; Kigoma Sisterz ya Kigoma, Simba Queens (Dar), Alliance Girls (Mwanza), Baobab Queens (Dodoma),  Mlandizi Queens (Pwani), JKT Queens (Dar), Panama (Iringa), Evergreen (Dar), Marsh Academy (Mwanza), Mapinduzi Queens (Njombe), Yanga Princess (Dar) na Tanzanite ya Arusha.

Comments are closed.