The House of Favourite Newspapers

Maalim Seif Akataa Kuitwa Msaliti

0

MAKAMU wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema uamuzi wa ACT-Wazalendo na yeye kuridhia kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitafa Zanzibar (SUK) usitafsiriwe kuwa ni usaliti kwa wananchi.

 

Jana Desemba 11, Maalim Seif ambaye ni mwenyekiti wa ACT-Wazalendo alizungumza katika mkutano uliofanyika makao makuu ya chama hicho Vuga, Mjini Unguja, na kukanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba yeye ni msaliti wa Wazanzibar kwa kukubali kuingia katika Serikali hiyo.

 

“Eti wapo wanaosema mimi ni msaliti kwa kukubali kuingia katika Serikali, kilichotokea si uamuzi wangu, bali ni uamuzi ya wananchi pamoja na kamati kuu. Mimi kama kiongozi mkuu wa chama kazi yangu ni kusimamia na nitaendelea kufanya hivyo kwa maslahi ya Wazanzibar,” alisema Maalim.

 

Desemba 8, 2020, Maalim Seif alikula kiapo cha kushika wadhifa huo mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, baada ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam kuja na uamuzi wa kuingia katika Serikali hiyo.

 

Hatua hiyo iliwagawa baadhi ya wapenzi, wafuasi na wanachama wa chama hicho, huku kwa nyakati tofauti Maalim Seif na Dk. Mwinyi wakieleza mikakati ya Zanzibar mpya, wakisisitiza maslahi mapana ya nchi hiyo.

 

Awali, chama hicho kilipinga mwenendo na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, kikidai kuwepo kwa matukio ya wanachama wake kuuawa na kuteswa.

.

Leave A Reply