The House of Favourite Newspapers

Mabadiliko ya Makocha Simba Yawe Chachu Ya Mafanikio

Kocha mpya mfaransa Pierre Lechantre.

SIMBA imepangua benchi la ufundi. Wameingiza sura mpya kuchukua nafasi ya Joseph Omog ambaye walimtimua hivi karibuni kwa maelezo kwamba hawakuridhika na ufanisi wake.

Makocha kadhaa wa Ulaya walihusishwa na Simba lakini Masoud Djuma atakuwa chini ya kocha mpya mfaransa Pierre Lechantre.

 

Maoni yetu Spoti Xtra ni kwamba mabadiliko yaliyofanyika yamezingatia masilahi ya maendeleo ya klabu. Hayakuwa ya kuwafurahisha mashabiki au kikundi fulani cha wanachama.

Uongozi wa Simba uliona kuna haja ya kuongeza nguvu, sasa ameletwa kocha mwenye utofauti na kile kilichozoweleka na kwa uzoefu wake anaweza kuisoma Simba haraka na kuongeza kitu cha ziada ndani ya muda mfupi.

Viongozi wa Simba wamechukua kocha mzuri ukiangalia wasifu wake ni mtu wa kazi.

Simba iko kwenye kipindi cha mpito ambacho wana mitihani miwili mikubwa.

Kikosi cha timu ya Simba.

Ule wa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara pamoja kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho linaloanza baadae mwezi ujao.

Ikumbukwe kwamba Simba tayari imeshatema ubingwa wake wa FA hivyo njia pekee ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Ambao ubingwa huo bado uko wazi kwa timu nyingi haswa Yanga, Singida, Mtibwa na Azam.

 

Simba wanahitaji kumlinda Masoud ili timu isitoke kwenye mstari wa mbio za ubingwa wakati makocha wapya waliokuja wakiendelea kusoma mazingira na kuweka sawa mipango kazi yao.

Maoni yetu ni kwamba Simba isifanye makosa ambayo yatawagharimu na kuwapotezea mwelekeo walionao. Kuondolewa kwenye mashindano ya Mapinduzi na FA ni jambo linalohitaji uvumilivu kwa klabu yenye wanachama na wanazi wengi kama Simba lakini bado viongozi wana nafasi ya kujitathmini na kufanya vizuri zaidi katika mashindano yaliyoko mbele yao.

Kama waliamua kufanya mabadiliko hayo ya benchi la ufundi bila shaka wamejiridhisha zaidi na zaidi kuhusiana na kile walichohitaji ili klabu ilete ushindani.

Maoni yetu ni kwamba klabu kama Simba au timu nyingine yoyote ile kati ya zile 16 inapokuwa makini na yenye ushindani, uimara wa ligi na mashindano yote unabadilika.

Na kama ligi ikiimarika inamaanisha kwamba nchi itapata bingwa imara ambaye ataondoa kasumba ya timu zetu kufanya vibaya tunapofika kimataifa.

Simba imemwajiri kocha mwenye jina kubwa Lechantre sasa itapaswa kumpa muda wa kuinua kiwango cha timu.

Wasifu wa Lechantre ni mkali kwani amewahi kuwa kocha bora wa mabara mawili ya Afrika na Asia.

Hatutegemei kuona mwalimu huyu anafanyiwa figisu katika kipindi hiki anafanya kazi ya kukiandaa kikosi cha Simba.

AJIBU ALIVYONG’ANG’ANIWA NA MASHABIKI

Comments are closed.