The House of Favourite Newspapers

MADAI MAZITO: POLISI AMPIGA RISASI RAIA MWEMA! – VIDEO

Hassan Yahaya akiugulia.

 

Haya ni madai mazito! Raia mwema aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Yahaya, mkazi wa Mabibo-Farasi jijini Dar, anadaiwa kupigwa risasi na askari mmoja wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu jijini Dar aliyetajwa kwa jina moja la Baraka, Risasi Jumamosi linaripoti.

 

NI WIKI MBILI TU BAADA YA AKWILINA

Tukio hilo linakuja ikiwa ni wiki mbili tu tangu lilipojiri tukio kama hilo la Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini kudaiwa kupigwa risasi na polisi waliokuwa wanawatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) maeneo ya Kinondoni-Mkwajuni, Dar waliokuwa wakielekea katika ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.

 

NI MABIBO-FARASI

Katika tukio hilo lingine baya lililojiri Februari 26, mwaka huu, maeneo ya Mabibo-Farasi, ilidaiwa kuwa, Hassan na wenzake ambao wote ni Polisi Jamii, wakiwa wanafanya ulinzi shirikishi katika eneo lao hilo, walipata taarifa kuwa nje ya Geti Namba Tatu la Shule ya Sekondari ya Loyola kulikuwa na tukio la unyang’anyi wa pikipiki almaarufu bodaboda.

Ilidaiwa kuwa, baada ya kupata taarifa hiyo ya uhalifu, ilibidi Hassan na wenzake waende Kituo Kidogo cha Polisi cha Mabibo-Mwisho jijini Dar kisha kutoa taarifa na kuomba kuongezewa nguvu.

Jeraha alipopigwa risasi.

 

 

TAHADHARI

Habari zilizopatikana kituoni hapo zilidai kuwa, jamaa hao walipofika kituoni hapo hakukuwa na askari wa ziada hivyo mkuu wa kituo hicho kwa muda huo aliwaambia waende kwa tahadhari na kuangalia kama wanaweza kuwakabili wahalifu hao.

HASSAN ASIMULIA MKASA MZIMA

Akilisimulia gazeti la Risasi Jumamosi mkasa mzima, Hassan alidai kuwa, walipoambiwa waende bila msaada wa polisi, waliamua kupita njia za vichochoro kuelekea eneo la tukio.

Alidai kuwa, walipofika kwenye nyumba moja iliyopo karibu na Shule ya Msingi Umoja, Mabibo, walikuta nyumba moja ina msiba.

 

Hassan alidai kuwa, kile kitendo cha kutokeza kwenye nyumba hiyo, walishtukia wakiitiwa wezi na kumuona askari huyo akimfyatulia risasi iliyomlenga mguuni.

“Ukweli nilipata maumivu makali sana na kuanguka hapohapo maana katika maisha yangu sikuwahi kuujua uchungu wa risasi inapoingia mwilini.

“Nikiwa nimeanguka, yule askari na mtu mwingine aliyedaiwa kuwa naye ni Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, kwa pamoja walianza kutushurutisha wakituita wezi.

Akiwa amepumzika.

 

 

MATESO

“Kwa kuwa wao (askari) walikuwa na silaha ya moto, ilibidi wenzangu wote ambao walikuwa na silaha za jadi za kulindia ulinzi shirikishi washindwe kufanya lolote na kukubali mateso tuliyokuwa tukipewa.

“Wakati wakiendelea kutuhenyesha, tuliwaambia kuwa kama sisi ni wahalifu, basi watupeleke polisi kwa maana walikuwa tayari wameshatudhibiti.

“Kweli baada ya muda walitufunga kamba na kutuswaga kama wahalifu hadi kituo cha polisi (Mabibo- Mwisho) huku mimi nikipata shida kutembea kutokana na jeraha la risasi lililokuwa likivuja damu.

“Walipotufikisha Kituo Cha Polisi cha Mabibo-Mwisho, mkuu wa kituo alipotuona, alishangaa kutuona tukifikishwa kituoni hapo tukiwa hoi kwa kipigo huku mimi nikiwa na jeraha la risasi.

“Yule afande aliyenipiga risasi alipoanza kutoa maelezo kuwa sisi ni majambazi, mkuu wa kituo alimkatisha kwa kumweleza kuwa sisi ni ulinzi shirikishi na tulikuwa tunawahi kwenye tukio la wizi wa bodaboda.

“Mkuu wa kituo hicho alimuuliza kama ukiachana na hilo tukio la wizi wa bodaboda hapo Loyola, yeye alikuwa akiwatuhumu kwa tukio gani lingine?

“Yule polisi hakuweza kulibainisha hilo,” alidai Hassan kwa uchungu.

 

MAGOMENI

Majeruhi huyo aliendelea: “Baada ya maelezo kituoni hapo, kesi hiyo ilihamishiwa katika Kituo cha Polisi cha Magomeni ambapo kesi ya kunipiga risasi ilifunguliwa katika jalada lenye namba MAG/RB/1863/2018- KUJERUHI.

“Ukumbukwe sasa hapo kulikuwa na kesi mbili, ya kwangu na ile ya kujeruhiwa pamoja na wenzangu ambayo ilifunguliwa katika jalada lenye namba MAG/RB/1866/2018- SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI.

“Baada ya hapo nilipewa Fomu Namba Tatu (PF-3) kwa ajili ya matibabu ambapo niliwahishwa Hospitali ya Mwananyamala. Wakati ninapata matibabu, polisi huyo alikuja na kutaka kuniona.

“Mimi nilikataa kuonana naye wala kuzungumza naye chochote kwa kuwa bado nilikuwa na maumivu makali.”

 

HUYU HAPA MTUHUMIWA

Baada ya kumsikia majeruhi huyo, mwandishi wetu alizungumza na mtuhumiwa huyo (Baraka) ambaye baada ya kusomewa madai hayo, alimuomba mwanahabari wetu wakutane sehemu ili waweze kuzungumza vizuri na kudai isingekuwa vizuri kuzungumza kwenye simu.

Mwandishi wetu alimtaka afande huyo kufika ofisi za gazeti la Risasi Jumamosi na kuahidi kufanya hivyo, lakini hakufika.

Kamanda Murilo.

 

 

KIONGOZI WA ULINZI SHIRIKISHI

Kwa upande wake kiongozi wa ulinzi shirikishi wa maeneo hayo, Primo Paul Mbutuli alithibitisha kutokea kwa tukio hilo katika eneo lake.

 

KAMANDA MAMBOSASA

Kufuatia sakata hilo, gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa ambapo simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisema afande huyo alikuwa kwenye kikao.

 

KAMANDA MULIRO

Baada ya kumkosa kamanda huyo, mwandishi wetu alimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Jumanne Muliro ambapo alirudisha ujumbe kuwa asingeweza kupokea simu muda huo na kuomba apigiwe baadaye.

Alipotafutwa baadaye, Kamanda Muliro alirudisha ujumbe mwingine kuwa yuko bize kwa muda na kumtaka mwandishi kumtumia ujumbe.

Mwandishi wetu alimtumia ujumbe kumwelezea tuhuma hizo, lakini Kamanda Muliro hakuujibu.

 

NINI HATMA?

Mwandishi wetu, sambamba na kumtumia ujumbe huo Kamanda Muliro, pia alimtumia Kamanda Mambosasa ambaye naye hakujibu hivyo tunaendelea kufuatilia kujua undani na hatma ya sakata hilo.

Stori: Richard Bukos, Risasi Jumamosi | DAR ES SALAAM

Aliyepigwa Risasi na Polisi, Asimulia Mazito!

Comments are closed.