The House of Favourite Newspapers

Maelfu Washiriki Mazishi ya Viongozi 12 Waliouawa kwa Shambulio

0
Walinzi wa heshima walibeba majeneza ya maafisa wa serikali ya Houthi waliouawa katika shambulio la anga la Israel, wakati wa maandamano ya mazishi yaliyofanyika jijini Sanaa, Yemen, Septemba 1, 2025.

Maelfu ya waombolezaji walikusanyika katika Msikiti mkubwa wa Al Saleh, jijini Sanaa — mji mkuu wa Yemen — siku ya Jumatatu, kuhudhuria mazishi ya viongozi 12 waandamizi wa kundi la Houthi, wakiwemo Waziri Mkuu wao, waliouawa katika shambulio la anga la Israel wiki iliyopita.

Shambulio hilo lililotokea Alhamisi iliyopita lililenga kundi kubwa la watu waliokuwa wamekusanyika kutazama hotuba ya televisheni iliyorekodiwa ya kiongozi mkuu wa Houthi, Abdul Malik al-Houthi. Tukio hilo limesababisha vifo vya karibu baraza zima la mawaziri wa kundi hilo, likiwa ni shambulio la kwanza la aina hiyo kuwalenga maafisa wa juu kabisa wa Houthi tangu kuanza kwa mvutano kati ya kundi hilo na Israel.

Naibu Waziri Mkuu wa serikali inayoongozwa na waasi wa Houthi nchini Yemen, Muhammad Ahmed Miftah, ambaye kwa sasa amepewa nafasi ya kuwa Kaimu Waziri Mkuu wa serikali hiyo, alihutubia wananchi wakati wa maandamano ya mazishi ya maafisa wa serikali ya Houthi waliouawa katika shambulio la anga lililofanywa na Israel, jijini Sanaa, Yemen, Septemba 1.

Waombolezaji walioshuhudia mazishi hayo walionekana wakipaza kauli mbiu ya kundi hilo isemayo: *”Mungu ni Mkubwa, Kifo kwa Marekani, Kifo kwa Israel, Laana kwa Wayahudi, Ushindi kwa Uislamu”*. Wakati huo huo, Mohammed Miftah — ambaye sasa ndiye kiongozi wa serikali ya Houthi inayoegemea Iran — aliahidi kulipiza kisasi na kufanya msako mkali dhidi ya kile alichokitaja kuwa mitandao ya ujasusi ndani ya Yemen.

 

Leave A Reply