The House of Favourite Newspapers

Mafaili ya Wagonjwa Yanaswa kwa Daktari Feki

HOFU imetanda katika Jiji la Mbeya na vitongoji vyake baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kumkamata Abdallah Shaibu Shija (42), anayedaiwa kuwa ni daktari feki akiwa na mafaili zaidi ya mia moja ya wagonjwa anaodaiwa kuwatibu.

 

Shija ambaye ni Mkazi wa Igodima jijini Mbeya alikutwa na mafaili hayo baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kufanya kazi za utabibu bila kuwa na taaluma ya utabibu hususan kwa magonjwa ya wanawake wenye matatizo ya uzazi.

 

Baadhi ya wanawake waliodai kutibiwa na Shija waliliambia Risasi Jumamosi kwamba, wamechanganyikiwa kwa sababu wameshapewa dawa na kuzitumia wakiamini kwamba mtu huyo ni mtaalam wa tiba za binadamu.

 

“Unajua dawa ni sumu, ukitumia bila kuzingatia utaalam, sasa kwa kuwa tumepewa na mtu ambaye Serikali inasema siyo daktari, tunakuwa na hofu kwamba tunaweza kupata madhara siku zijazo,” alisema mama mmoja aliyedai kutibiwa na Shija huku akiomba hifadhi ya jina lake.

 

Neva Kafwila ni Mkazi wa Isyesye, Mbeya ambaye alisema wananchi waache kutibiwa hovyo mitaani kwani wanahatarisha maisha yao.

Hata hivyo, aliiomba Serikali kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa watoa huduma za afya kwa sababu wananchi siyo rahisi kujua kama daktari anayewahudumia ni feki au la.

 

Mwanamke mwingine aliyewahi kutibiwa na Shija alisema anakuwa na hofu na tiba aliyopewa kwa sababu baada ya tiba badala ya ugonjwa kupungua, umeongezeka na sasa anasikia maumivu makali ya tumbo.

 

Mwanamke huyo aliiomba Serikali, wote waliotibiwa na Shija wafanyiwe vipimo upya ili kuona kama dawa walizopewa na kuzitumia hazijawaletea madhara.

 

Naye Mashaka Sanga, Mkazi wa Simike jijini Mbeya alisema mara nyingi huduma za afya zinazotolewa mitaani nyingi zinakuwa si sahihi, hivyo Serikali inawajibika kugundua hilo kabla ya madhara kutokea.

 

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk Jonas Lulandala alisema wananchi waache kuweka rehani maisha yao kwa kwenda kutafuta huduma za tiba kwa watu wasio sahihi kama Shija.

 

Dk Lulandala alisema baadhi dawa zilizokutwa kwa daktari huyo feki zilikuwa zimemalizika muda wa matumizi jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

 

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei alisema Shija alikamatwa Juni 24, mwaka huu, majira ya saa 7:50 mchana baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanawake watano maeneo mbalimbali jijini Mbeya.

 

Kamanda Matei alisema; “Katika mahojiano na mtuhumiwa, alikiri kuwatapeli wananchi kiasi cha shilingi 2,472,000/= kwa madai kuwa atawasaidia kutatua matatizo ya uzazi yakiwemo ya kupata ujauzito ambapo alishindwa kuwatatulia matatizo yao.

 

Aliongeza kuwa, baada ya kumpekua mtuhumiwa alikutwa na vitu mbalimbali zikiwemo dawa za Serikali, vipimo mbalimbali vya kupimia ujauzito na nguo ya udaktari.

 

“Baadhi ya vitu vilivyokamatwa nyumbani kwa mtuhumiwa ni fomu za maabara, vipimo na kadi za hospitali na zahanati, kipimo kiitwacho Urine Pregnant Test 15, dawa ya kusafishia vidonda, spiriti, Iodine, kipimo cha malaria (MRDT), glucose iliyokwisha muda wake, dawa ya metronidazole za Serikali (MSD), dawa za ganzi, nyembe, BP Digital Machine, kipimajoto, Syringe 89, Clinical Coat, groves, picha za X-ray na mafaili 119 ya wagonjwa,” alisema Matei.

 

Alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa pale wanapowashuku watu wanaotoa huduma za afya kinyume cha sheria na akasema uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika Shija atapelekwa mahakamani.

 

STORI: EZEKIEL KAMANGA, Mbeya

Comments are closed.