JPM Atua Kwenye Daraja Moro, Asimamisha Kazi Wahandisi 12, Amuonya Waziri – Video
RAIS John Magufuli leo amewasimamisha kazi wahandisi 12 wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Morogoro na kuwapa onyo la mwisho Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Isack Kamwelwe; Mtendaji Mkuu TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale na Mkurugenzi wa Matengenezo wa wakala huo kwa uzembe uliosababisha kuvunjika kwa daraja la Kiegeya mkoani humo.
Magufuli amefanya uamuzi huo leo, Jumatatu, Machi 16, 2020, alipotembelea neo la daraja hilo kushuhudia lilivyosombwa kwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha kukatika mawasiliano kati ya Dodoma na Morogoro.
“Sitaki kuona barabara ya mkoa au kuu imefungwa kwa sababu daraja limekatika, sitaki kusikia hilo kutoka kwa TANROADS wote Tanzania nzima kwa sababu nafahamu fedha za kufanya ‘maintenance’ zipo, haiwezekani daraja mpaka likatike ‘engineer’ (mhandisi) upo na fedha unazo. Kila barabara ikikatika katika mkoa, yule Regional Manager ajihesabu hana kazi,” amesema Magufuli.



