The House of Favourite Newspapers

Mahakama ya Juu Kenya Yamzuia Rais Kubadili Katiba

0

MAHAKAMA ya Juu nchini Kenya imeamua kwamba mageuzi ya kikatiba yanayoungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga ni kinyume na sheria, uamuzi unaompa nguvu Naibu Rais William Ruto.

 

Katika uamuzi wake jana Mei 13, Mahakama hiyo ilisema rasimu ya sheria ya mabadiliko ya katiba, maarufu kama Building Bridge Initiatives (BBI), ni hatua binafsi ya Rais Kenyatta ambaye hana mamlaka ya kisheria kuanzisha mchakato wa mabadiliko yoyote ya kikatiba kupitia uhamasishaji wa umma.

 

Mpango huo ambao umeligawa taifa hilo la Afrika Mashariki kisiasa, unapendekeza kuuondoa mfumo wa mshindi wa uchaguzi kuchukuwa kila kitu, jambo ambalo Rais Kenyatta anasema limechochea migogoro ya kila baada ya uchaguzi.

 

Tayari bunge la taifa lilishayapitisha marekebisho yaliyopendekezwa ambayo yanaashiria mabadiliko makubwa kabisa kwenye mfumo wa serikali tangu katiba mpya kupitishwa mwaka 2010.

 

Lakini wakitoa uamuzi kutokana na mapingamizi kadhaa yaliyowekwa na makundi mbalimbali nchini Kenya, majaji watano wa Mahakama hiyo ya Juu walisema “Kenyatta alitumia kipengele cha katiba kilichowekwa kwa ajili ya raia kuanzisha mabadiliko hayo”, na hilo linaifanya hatua yake kutokuwa na uhalali wa kisheria.

 

“Rais hawezi kuwa mchezaji na muamuzi kwa wakati mmoja.” Alisema Jaji Jairus Ngaah akisoma uamuzi huo

Serikali, ambayo inataka kuitisha kura ya maoni baada ya Kenyatta kuusaini muswaada huo kuwa sheria, ilisema ingeliukatia rufaa uamuzi huo wa Mahakama ya Juu.

Leave A Reply