The House of Favourite Newspapers

Mahakama Yatengua Hukumu ya Kina Mwana FA, AY

0

MAHAKAMA Kuu, Dar es Salaam, imetengua hukumu iliyoiamuru kampuni ya simu za mkononi MIC (T) Limited, maarufu Tigo, kuwalipa wanamuziki wa kizazi kipya, Hamisi Mwinyijuma (Mwana-FA) na Ambwene Yesaya (AY) Sh 2.1 bilioni kwa kukiuka sheria za hatimiliki.

 

Jaji Joacquine De-Mello amebatilisha uamuzi huo baada ya kukubaliana na rufaa ya Tigo kuwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala haikuwa na mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo.

 

Uamuzi huo unakuja huku tayari wanamuziki hao maarufu wa muziki wa Bongo Fleva wakiwa wametia fedha hizo kibindoni baada ya vita kali ya kisheria kati yao na Tigo ambayo ilipinga kwa nguvu zote kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo bila mafanikio.

 

Kampuni hiyo ililazimika kulipa pesa hizo baada ya wasanii hao kuikaba kooni kwa kukamata akaunti zake baada ya kupata amri ya Mahakama ya Ilala, kufuatia maombi yao ya utekelezaji wa hukumu hiyo baada ya kampuni hiyo kuchelewa kulipa.

 

Wakati ikiwalipa fedha hizo, kampuni hiyo tayari ilikuwa imeshafungua maombi mahakama, ikiomba kibali cha kukata rufaa nje ya muda na baada ya kufanikiwa kupata kibali hicho ndipo ikakata rufaa hiyo.

 

Wakili wa kampuni ya Tigo, Rosan Mbwambo, amesema kuwa atawaandikia barua wasanii hao kuwataka warejeshe fedha walizolipwa na mteja wake.

 

Leave A Reply