The House of Favourite Newspapers

Maisha Magic Movies Yatangaza Neema Kwa Filamu Tanzania

0

Chaneli maarufu ya Maisha magic Movies imetangaza neema kwa wazalishaji wa filamu hapa nchini baada ya kuongeza idadi ya filamu za kitanzania zinazorushwa katika chaneli hiyo.

Katika kunogesha uhundo huo zaidi, Kampuni ya MultiChoice imetangaza kuwa sasa chaneli hiyo inapatikana kuanzia kifurushi cha DStv Bomba ambavyo ni miongoni mwa vifurushi vya chini hivyo kuwawezesha wateja wengi zaidi hususan wenye kipato cha chini kufurahia burudani ya tamthilia, filamu za kawaida, vitimbi, vichekesho na kazi nyingine nyingi za wasanii wetu  katika kifurushi cha DStv Bomba ambacho hupatikana kwa Sh 21,000 tu kwa mwezi.

Akizungumza katika hafla maalum ya chaneli hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Baraka Shelukindo amesema kuwa hapo awali chaneli hiyo maarufu ya filamu za ukanda wa Afrika Mashariki ilikuwa ikipatikana katika kifurushi cha DStv Compact kwa Sh 51,000 kwa mwezi, lakini sasa imeshushwa hadi kwenye kifurushi cha DStv Bomba cha Sh 21,000 tu kwa mwezi.

“Kuwepo kwa chaneli hii kwenye vifurushi vya chini kutawafanya watanzania wengi zaidi kufurahia kazi na sanaa zetu kwani sasa mbali na chaneli ya Maisha Magic Poa na Maisha Magic Bongo, sasa chaneli hii nayo ipo katika vifurushi vya bei nafuu” alisema Baraka na kuongeza kuwa “mbali na kupanua wigo wa kutazamwa kwa kazi zetu, pia tumepanua wigo wa kuongeza kazi za wasanii wetu katika chaneli hizi. Hii inamaanisha kuwa tutachukua kazi nyingi zaidi na hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wasanii wetu na kuongeza mchango wetu katika kujenga uchumi wetu”

Miongoni mwa filamu za kitanzania zilizomo katika chaneli hiyo ni Pamoja na Frida na Mvamizi zilizoandaliwa na muandaaji mchanga Wilson Nkya, Uncle na Samaki kwa wote – Hatibu Madudu; Tego – William Mtitu; Malkia – Neema ndepanya; Alifu kwa Ujiti – Ayoub Bombwe; Rupia ya Kijerumani – Jamila Bakari; Ndoto Kubwa – Staford Kihore; Kama nitabaki na nyinginezo nyingi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Filamu wa bodi ya Filamu Tanzania Emmanuel Ndumkwa  amesema kuongezeka kwa chaneli zinazoonyesha filamu za Tanzania ni fursa adhimu kwa ukuaji wa sekta ya filamu hapa nchini. Emmanuel ameipongeza MultiChoice kupitia chaneli zake mahsusi za Maisha Magic Bongo, Maisha Magic Movies na Maisha Magic Poa ambazo zimekuwa zikionyesha filamu nyingi za kitanzania.

“Wasanii wetu watumie fursa hii vizuri kwani kuchukuliwa kwa kazi zao nyingi na DStv kunawaweka kwenye ulingo wa kimataifa pia hivyo zinaweza kupambanishwa na filamu za nje. Hii ni fursa ambayo tunapaswa kuitumia kukuza soko la filamu zetu nje na kuwafanya wasanii na wazalishaji wetu wapate faida kubwa kwa kazi zao za Sanaa” alisema Mkurugenzi huyo

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa Matiko Mniko, amesema baraza linatambua mchango mkubwa unaofanywa na DStv katika kukuza Sanaa ya Filamu hapa nchini na kusema kuwa kitendo cha chaneli ambayo imeanzishwa hivi karibuni kuchukua kazi zaidi ya 100 za watanzania ndani ya muda mfupi ni uthibitisho wa umuhimu wa chaneli hiyo katika ukuaji wa tasnia ya Sanaa ya filamu hapa nchini.

Kwa upande wao, baadhi ya wazalishaji wa filamu zinazorushwa na chaneli ya Maisha Magic Movies wamesema kuwa kuwepo kwa chaneli hiyo kumekuwa mkombozi mkubwa kwao kwani wamepata jukwaa la uhakika la kazi zao kuonekana ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Wilson Nkya ambaye ni mzalishaji wa filamu za Frida na Mvamizi ambazo zinaonyeshwa katika chaneli ya Maisha Magic Movies amesema kwa yeye mzalishaji mpya imekuwa ni Fahari kubwa kwa kazi zao kuweza kupata nafasi katika chaneli hii. “Mimi na wenzangu tulioshiriki kuzalisha filamu hizi ni chipukizi kwani baadhi yetu tumehitimu mafunzo yetu katika academy ya MultiChoice hivi karibuni. Hili ni jukwaa muhimu sana si kwetu tu, bali kwa wazalishaji na wasanii kwa Tanzania kwa ujumla” alisema Wilson na kuwashauri watanzania kutumia fursa ya kuwepo kwa chaneli hii kuongeza ubora katika uzalishaji na uandaaji wa filamu ili Tanzania iweze kushindana vyema katika soko la filamu la kikanda na la kimataifa.

Chaneli ya Maisha Magici Movies ilianzishwa mnamo Julai 28, 2021 ikiwa ni chaneli mahsusi kwa ajili ya filamu za Afrika Mashariki.

Awali chaneli hii ilikuwa ikipatikana katika kifurushi cha DStv Compact cha Sh 51,000 lakini sasa imeshushwa hadi kifurushi cha DStv Bomba cha Sh 21,000 tu!

Tangu kuanzishwa kwake chaneli hii imeshachukua filamu zaidi ya 100 (Mia moja) kutoka kwa wazalishaji mbalimbali wa Tanzania wakiwemo Wilson Nkya, Hatibu Madudu; William Mtitu; Neemba ndepanya;  Ayoub Bombwe; Jamila Bakari; Staford Kihore na wengineo

Leave A Reply