The House of Favourite Newspapers

MAMA, BINTIYE MATESO JUU YA MATESO

MAISHA ni changamoto! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Veronica Peter Kidava kujikuta kwenye wakati mgumu baada ya yeye na mwanaye kuwa hoi kwa magonjwa mazito.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mama huyo alieleza kuwa, kwa sasa yupo kwenye wakati mgumu kwani yeye anasumbuliwa na kansa ya titi ambapo amekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road iliyopo Dar na kwamba Agosti 10, mwaka huu ndipo atakapopangiwa tarehe ya kwenda Muhimbili kufanyiwa upasuaji. “Nina tatizo la kansa ya titi la kushoto ambapo inatakiwa shilingi laki tisa kwa ajili ya oparesheni, lakini mpaka sasa sijapata hata senti na sijui ninaipatia wapi,” alisema mama huyo.

Kama mateso ya mama huyo hayatoshi; mwanaye aitwaye Miriam Michael pia yupo kwenye hali mbaya, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na ameteseka nao kwa muda mrefu bila kuwa na msaada wowote.

“Nimeteseka na mwanangu kwa muda mrefu sana na sina msaada wowote ninaopata kutoka kwa ndugu au jamaa zangu, kwa kipindi chote nimekuwa nikihangaika mwenyewe, licha ya baba wa mtoto wangu kuwa hai lakini sijaona msaada wake,” alisema mama huyo huku akifunika macho yake yaliyokuwa yakibubujikwa machozi.

Aliendelea: “Mwanangu ameanza kusumbuliwa na tatizo hili la moyo akiwa na umri wa miaka 12 mpaka sasa ana miaka 17 kwa hiyo ni takriban miaka mitano sasa nahangaika naye bila mafanikio yoyote japokuwa alishawahi kufanyiwa Oparesheni hapahapa Muhimbili mwaka 2016, nilitoa shilingi milioni nne, kiasi nilitoa mwenyewe na kingine nilikusanya kwa kuombaomba.

“Alifanyiwa lakini kwa bahati mbaya hakupona, alipumzika mwezi mmoja tu baada ya hapo akaanza kuumwa tena, nikamrudisha hospitali, nimeambiwa tatizo lake kwa hapa nchini limeshindikana inabidi aende India kimatibabu,” alisema mama huyo kisha akashusha pumzi. Aliongeza kuwa, kiasi cha fedha kinachohitajika kwa matibabu ya mwanaye huko India ameambiwa ni shilingi milioni 25 ambazo hana.

“Sijui nifanye nini, nikimwangalia mwanangu nabaki nalia, nikijifikiria na mimi mwenyewe ndiyo hivyo najikatia tamaa, nahisi naishi kwenye dunia ya peke yangu. “Sina furaha, kuna wakati mwanangu naye ananililia mimi, naye hana la kufanya, tumekuwa watu wa kusubiri mapenzi ya Mungu,” alisema mama huyo kisha kufuta machozi tena.

Risasi lilipomuuliza kuhusu hatima yake, mama huyo alisema anaiomba serikali iingilie kati angalau isaidie kuokoa maisha ya mwanaye huku akiwaomba wasamaria wema wajitokeze. “Niko chini ya miguu ya kila Mtanzania mwenzangu, nawaomba wenye kidogo, watu wenye huruma na uhai wangu na mwanangu watusaidie kututoa katika maisha haya magumu,” alisema mama huyo.

Kwa yeyote aliyeguswa na matatizo mazito ya mama huyo anaweza kuwasiliana naye kwa namba zake zifuatazo 0719080199 au 0756160823- jina litatokea Veronica Peter Kidava. Waswahili husema kutoa ni moyo na wala si utajiri.

STORI: Shamuma Awadhi, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.