The House of Favourite Newspapers

Mambosasa: Abdul Nondo Alikwenda Iringa kwa Mpenzi Wake – Video

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa kauli kuhusu Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo (24) aliyedaiwa kutekwa wiki iliyopita, kuwa si kweli kwamba alitekwa, bali alisambaza taarifa za uongo na kwamba alikuwa anakwenda Iringa kumtembelea msichana mmoja ambaye jina lake halijawekwa wazi.

 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar.

 

“Huyu mwanafunzi aliyedai kutekwa si kweli, kuna mawasiliano ambayo tumeyakamata alikuwa akifanya na binti mmoja ambaye ndiye alikuwa anamfuata huko Iringa. Alipatikana akiwa mzima wa afya akiendelea na shughuli zake za kawaida, alipelekwa kwa daktari kupimwa na kukutwa hana tatizo lolote la akili.

 

“Baada ya kufanya uchunguzi tumebaini na kujiridhisha kuwa mwanafunzi huyo alikuwa huru na alifika Iringa akiwa salama. Huo muda anaosema alitekwa saa saba usiku, alikuwa bado anafanya mawasiliano ya meseji ya kawaida na huyo binti aliyekuwa anamtembelea huko Iringa.

 

“Tulitegemea alipoachiwa pengine angeenda kituo cha karibu cha polisi na kujieleza, lakini amekutwa katika mazingira kama nilivyoelezea…. huyu ni mhuni tu kama wahuni wengine. Pengine alilizua hilo ili kutaka kujipatia umaarufu,” alisema Mambosasa.

 

Aidha, Mambosasa amesema baada ya uchunguzi kuendelea walibaini Nondo alikwenda Iringa kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akifanya naye mawasiliano ya mara kwa mara wakati akiwa njiani kwenda Iringa, hivyo jeshi hilo linaendelea kumshikilia.

VIDEO: MSIKIE MAMBOSASA AKIFUNGUKA

Comments are closed.