The House of Favourite Newspapers

Mapya Yaibuka, Zari Kujenga Hospitali ya Wanawake Dar

MIONGONI mwa mambo ya kumfanya staa akumbukwe hata baada ya kifo chake ni pamoja na kurudisha kwa jamii (to give back to community) kwa kusaidia watu wenye uhitaji wa huduma fulanifulani.

Kufanya kazi nzuri ya sanaa, hiyo pekee haitoshi kukumbukwa kwa miaka yote, bali harakati za kusaidia jamii kama afanyavyo mwanamama mjasiriamali Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.

Mwanamitindo huyo kutoka Uganda na ambaye anaishi nchini Afrika Kusini ‘Sauz’ ni mzazi mwenza wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

ZARI ASHTUA WABONGO

Katika harakati za kurudisha kwa jamii kile anachokipata hata kama ni kidogo kupitia burudani, ujasiriamali na uanamitindo, Mwanamama Zari ambaye amepata umaarufu mkubwa katika nchi zote za UTAKE (Uganda, Tanzania na Kenya), ameshtua Wabongo wengi baada ya kuweka wazi mpango wake wa kujenga hospitali kubwa ya wanawake jijini Dar nchini Tanzania.

Zari alianza kutambulisha wazo lake hilo baada ya kuposti picha akiwa amevalia vazi la harusi kwenye akaunti yake ya Mtandao wa Instagram kisha kuwashukuru wafuasi wake (followers) wa Bongo kwa kufanikiwa kufikisha wafuasi milioni 4.

DOLA 1 KWA KILA MFUASI

Kupitia posti yake hiyo, Zari aliwaomba kila mfuasi kutoa mchango wa dola moja ya Kimarekani ili kufanikisha ujenzi wa hospitali hiyo ya akinamama jijini Dar.

Aliandika: “Wapendwa wangu sina cha kuwalipa zaidi ya kusema asanteni sana kwa kufikisha wafuasi milioni 4.

 

“Ninyi ni ndugu kwangu, mmekuwa nami bega kwa bega, kwenye shida na raha. Sasa mnichangieni dola 1 kila mtu ili tujenge kliniki ya wanawake sehemu yoyote Dar.

“Najua tukiipata (hiyo pesa), Baba Magufuli (Rais John Pombe Magufuli) atatupa kiwanja, nawapenda sana ninyi.”

 

HESABU ZINASEMAJE?

Kama kweli kila mfuasi wake atatoa kiasi hicho cha dola moja, basi Zari atakusanya kiasi cha shilingi bilioni 9.05 kwa ajili ya ujenzi huo ambao utakuwa ni kufuru jijini Dar.

Baada ya mwanamama huyo kuweka mambo hayo ambaye kwa mujibu wa watu wake wa karibu ni mpango wake wa muda mrefu, mambo yalikuwa ni moto ambapo baadhi ya wafuasi wake waliomba kupewa utaratibu wa namba ya kuchangia huku wengine wakiahidi kutoa zaidi kutokana na wazo lake hilo zuri.

“Unajua Zari anakubalika sana Bongo, ndiyo maana anatamani kuweka kabisa makazi. Naona ameanza kwa kujitolea kwenye jamii.

“Baadhi ya watu wanauliza kwa nini asijenge nyumbani kwao nchini Uganda? Lakini ukweli ni kwamba alishajitolea sana na huwa ana vituo vyake vya yatima ambavyo huwa anavihudumia.

“Kuhusu Kenya, juzijuzi alikuwa huko kujitolea kuhamasisha wasichana dhidi ya kujilinda na kansa ya uzazi na kutembelea vituo mbalimbali vya watu wanaohitaji misaada,” alifunguka mtu huyo wa karibu wa Zari.

 

HUYU HAPA FELLA

Kwa mujibu wa mmoja wa mameneja wa Diamond, Said Fella, alisema kuwa anaamini jambo hilo limepokelewa kwa mikono miwili kwani anafurahishwa mno na watu wanaomuunga mkono katika kutatua kero za wananchi.

Fella alifunguka kuwa, naye kama Diwani wa Kata ya Kilungule wilayani Temeke, Dar, yupo tayari kumuunga mkono Zari huku akilifanyia kazi ombi lake la kiwanja kutoka kwa Magufuli kwa kuahidi kumpa kiwanja kwenye kata yake na kwamba hata akihitaji kiwanja chenye ukubwa kiasi gani, atajipanga na wananchi wake au hata atampa cha kwake.

“Nimefurahishwa sana na mpango wa Zari. Sisi tupo tayari kumpa sapoti atimize lengo lake.

“Hata mimi kama mimi kwenye kata yangu ya Kilungule, nina uwezo wa kumpatia kiwanja kikubwa ili tupate hiyo hospitali.”

 

TUJIKUMBUSHE

Miezi kadhaa iliyopita Diamond ambaye amezaa watoto wawili na Zari, Tiffah na Nillan, naye alitangaza mipango yake ya kujenga hospitali kubwa ya matatizo ya moyo katika mtaa aliokulia wa Tandale jijini Dar, mipango ambayo bado haijaonesha hata dalili.

 

MSIKIE DIAMOND

“Mafanikio yote tunayopata hatusahau kurudisha kwa jamii kile tunachokipata. Ukiachana na misikiti ambayo nimekuwa nikiijenga katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania habari nje kwa ndugu zangu wa Tandale ni kwamba nataka kuwajengea hospitali ambayo itakuwa inatoa huduma pale kwa bei nafuu.” Alisema Diamond.

Comments are closed.