The House of Favourite Newspapers

MASTAA WALIOSHAINI WAKILELEWA NA MAMA TU

Vincent Kigosi ‘Ray’,

MASTAA wengi duniani wamekuwa wakishaini na kuvuta mkwanja mrefu, ukiuliza undani wa malezi yao utaambiwa kuwa wametoka migongoni mwa mama zao kwa maana ya kulelewa.

Kweli! Hili siyo la mastaa wa Tanzania tu bali kwa waliofanikiwa kusoma wasifu wa mastaa mbalimbali wa nje wengi wao wamelelewa na mama zao pekee bila baba lakini wamefikia mafanikio makubwa na kushaini. Wengi huwa ni mastaa ambao aidha wamefiwa na baba au wanalelewa na mama peke yake huku baba akiwa na familia nyingine au wakati mwingine wakiwa wametengana na mama zao. Hawa hapa chini ni baadhi ya mastaa ambao wamelelewa na mama zao; 

Aunty Lulu

Huyu hapa Lulu Semagongo ‘Aunty Lulu’ ametokea kwenye utangazaji akiwa anatangaza kipindi cha watoto lakini pia alivuma sana aliposhinda Shindano la Kimwana Manywele na kujiingiza kwenye uigizaji. Naye ni zao kutoka kwa mama yake, baada ya baba yake kufariki alilelewa na mama yake na mafanikio yake ya kuwa maarufu ameyapata akiwa mikononi mwa mama yake mzazi.

Akiongea na Risasi, Aunty Lulu alisema kuwa mama yake ni kila kitu kwake amemlea na kumsomesha lakini mafanikio yote aliyonayo bila mama yake asingefika pale alipo kwani hata alipokwenda ndivyo sivyo mama yake alikuwa akimsema sana na mpaka sasa ametulia.

Nay wa Mitego /Ray

Mastaa wengine ni pamoja na Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ na Vincent Kigosi ‘Ray’, mastaa hawa ni miongoni mwa watu maarufu ambao wamelelewa na mama zao na kushaini. Nay mara nyingi amekuwa akisifia uwepo wa mama yake ambaye humuita mwanamke wa chuma. “Mama yangu ni mwanamke wa chuma sina cha kumlipa zaidi ya kumuombea dua, amenitoa mbali.” Ray amekuwa na mama yake mwanzo mwisho wa malezi yake ambapo mpaka sasa anaishi nyumbani kwake tofauti na mastaa wengine ambao huamua kufuata maisha mengine nje ya wazazi wao.

Alisikika akidai kuwa amekuwa akikaa nyumbani kwa mama yake kwa sababu haoni sababu ya kwenda kujitegemea wakati nafasi ya kuishi kwao ipo. “Kukaa na mama yangu sioni tatizo kwani hata hivyo maisha yote amekuwa msaada mkubwa kwangu kuanzia malezi na mafanikio yangu ni kwa dua zake yeye, nampenda,” alisema Ray.

Yvonne Cherrie ‘Monalisa

Wengi tunamjua kwa jina la Monalisa hatujawahi kumsikia wala kumuona akiwa na baba yake hata kwa kumtaja wala kueleza chochote kuhusiana na maisha yake halisi hasa ya mafanikio yake. Mama yake Suzan Lewis ‘Natasha’ amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mwanaye anakuwa kistaa.

Kwa kiasi kikubwa amefanikiwa kumfikisha mbali kwani kando na kumkuza kisanaa lakini amefanikiwa kucheza naye kwenye michezo mbalimbali ikiwemo tathilia ya Mambo Hayo na filamu mbalimbali, wamekuwa kivutio kila wanapokwenda kwani huongozana. Wapo wanaodhani ni mtu na mdogo wake.

Monalisa akimuongelea mama yake mara nyingi husema haya: “Mama yangu ni rafiki yangu wa karibu, amekuwa mstari wa mbele kila wakati, kwenye shida na raha.” Lakini pia humsifia sana mama yake kwa kumuita, mpambanaji, mcheshi, mcha Mungu, mwenye upendo na mwenye subira, akisisitiza kuwa ni mama ambaye mara nyingi humsamehe hata pale anapomkosea.

Wema Sepetu

Wema Sepetu naye ni miongoni mwa mastaa ambao ni watoto wa mama, mama yake amekuwa karibu naye muda mwingi alianza kwa kumuingiza kwenye tasnia ya urembo akawa Miss Tanzania akitokea Kinondoni.

Mbali na hapo mama yake amekuwa akimsapoti kwenye suala zima la uigizaji, mara nyingi amekuwa akionekana kwenye uzinduzi wa filamu zake hata akiwa na misala ya kuitwa mahakamani huongozana naye lakini pia akiwa kwenye masuala ya furaha pia huongozana naye. Kutoka kinywani kwake Wema amedai kuwa; “Mama yangu hajawahi kuniacha amekuwa mama bora siku zote kwangu, kuna wakati namuonea huruma lakini nampenda na nitakuwa mtoto bora kwake.”

Elizabeth Michael ‘’Lulu’’

Ni staa wa filamu za Kibongo, kwa mara ya kwanza kabisa alitokea kwenye Kundi la Kaole kwenye mchezo wa Zizimo na baada ya hapo alicheza michezo mingine kama vile Baragumu, Gharika na Taswira ambapo aliyempeleka kwenye kundi hilo ni mama yake akiwa na umri enzi hizo Lulu akiwa na miaka mitano na kumkabidhi kwa msanii Muhsein Awadh ‘Cheni’ na kuanza kuigiza na mpaka sasa ukilitaja jina lake utakuwa umetaja muigizaji maarufu Bongo.

Bila kificho mama wa Lulu amekuwa akimshika bega mwanaye pale anapolia, anapocheka na hata anapopita kwenye magumu ya aina yoyote. Amemlea akiwa peke yake mpaka sasa wamekuwa wakiishi pamoja. Mwanamuziki Gift Stanford ‘Gigy Money’ naye ni miongoni mwa mastaa waliotokea mikononi mwa mama.

Mama wa msanii huyo alimuongelea mwanaye na kudai kuwa baada ya kuwa mbali na baba yake amemlea mwenyewe lakini alipokuwa katika makuzi yake aligundua kuwa ana fani flani kwani alikuwa akipenda kuvaa nguo fupi na kujipiga picha hivyo alivyoamua kuingia kwenye U-video Queen kwa mara ya kwanza hakuona sababu ya kumzuia kwani hata yeye alikuwa hivyo na aliamini kuwa mtoto akiwa na kipaji aachwe afanye kwa hiyo alimsapoti.

“Unajua mwanangu Gigy anapitia yale niliyoyapitia mimi kwani nilibaini ana kipaji tangu akiwa na umri mdogo na ninashukuru kipaji chake sasa kinaonekana, amekuwa video queen na sasa anaimba muziki. Mtoto akiwa na kipaji unatakiwa kumuacha akifanyie kazi,” alisema mama huyo.

Comments are closed.