The House of Favourite Newspapers

Maswali 8 Tata Kumhusu Scorpion

uwazi-1

Na Waandishi Wetu, Uwazi.

Dar es Salaam: Tukio la ukatili wa kupindukia aliotendewa kijana Said Mrisho akidaiwa kuvamiwa, kuchomwa visu na bisibisi, kutobolewa macho na kuporwa fedha, bado linaendelea kusumbua vichwa vya wengi, huku mtuhumiwa Salum Henjewele ‘Scorpion’ aliyepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Jumatano iliyopita, akiibua maswali nane tata kumhusu.

SCORPION CHINI YA ULINZI: Mtuhumiwa wa unyang'anyi wa kutumia silaha, Salum Njwete maarufu 'Scorpion' akisindikizwa chini ya ulinzi wa polisi na askari magereza kuelekea kwenye basi la magereza kurudishwa rumande huku akicheka baada ya waandishi kubaini mbinu zake za kubadilisha nguo ili wasimtambue baada ya kusomewa shitaka lake katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam jana. Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumvamia na kumtoboa macho mkazi mmoja wa Dar es Salaam hivi karibuni. (Na Mpigapicha Wetu).Mtuhumiwa Salum Henjewele ‘Scorpion’.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, timu ya waandishi makini wa Gazeti la Uwazi, imeingia mtaani kuchimba kwa kina kuhusu tukio hilo na mtuhumiwa wake, Scorpion na yafuatayo ni maswali nane tata yalioibuka, yakimhusu Scorpion.

ALIJISALIMISHA  MWENYEWE AU ALIKAMATWA?

Swali la kwanza ambalo linasumbua vichwa vya wengi, ni kuwepo kwa mkanganyiko wa taarifa za jinsi mtuhumiwa huyo alivyotiwa mbaroni. Wakati taarifa za awali zikionesha kwamba Scorpion alikamatwa na polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Stakishari katika msako mkali ulioendeshwa baada ya tukio hilo, habari mpya zinadai kuwa alijisalimisha mwenyewe polisi.

Kaizile Jabiry, ni mwalimu wa karate wa Scorpion ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita, alifika kwenye ofisi za gazeti hili na kuzungumza mambo mengi kumhusu mtuhumiwa huyo. Miongoni mwa mambo aliyoyazungumza, ni kwamba mtuhumiwa huyo alijisalimisha mwenyewe polisi baada ya kusikia kwamba anasakwa na siyo kweli kwamba alikamatwa.

“Kwa maelezo ambayo ninayo, Salum (Scorpion) alijipeleka mwenyewe kituo cha polisi cha Stakishari na kujisalimisha baada ya kusikia kwamba anatafutwa mitaani,” alisema Kaizile.

WADAU WAKE HAWALIJUI JINA LA SCORPION

Jina la Scorpion lilianza kuvuma tangu siku ya tukio, watu mbalimbali wakimtaja kwamba ndiye mhusika wa ukatili huo na kwamba alikuwa maarufu mitaa yote ya Buguruni lilikotokea tukio hilo.

Hati ya mashtaka aliyosomewa mtuhumiwa huyo, ikamtaja ‘Scorpion’ kwamba jina lake halisi ni Salum Henjewele. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ukiwahusisha watu wake wa karibu, unaonesha kwamba ‘Scorpion’ siyo jina lililokuwa likitumiwa na Salum Henjewele kama watu wengi wanavyofahamu.

A.K.A YAKE NI SAM JET!

Kuhusu hilo, mwalimu wake wa mafunzo ya Karate, Kaizile anasema: “Hilo jina la Scorpion mimi nimeanza kulisikia kwenye magazeti na vyombo vya habari lakini kabla ya hapo sikuwa nalifahamu. Sisi tulizoea kumuita kwa jina la utani la Sam Jet na hilo ndiyo watu wake wote wa karibu wanalolifahamu.”

Mtayarishaji mkongwe wa sinema Bongo, Tuesday Kihangala ‘Mr. Chuz’ ambaye inadaiwa kwamba Scorpion alikuwa msanii wa kundi lake la sinema za kibongo, akishiriki kwenye tamthiliya za Philipina na Milosis, naye anasema kwamba anamfahamu vizuri Salum lakini hakuwahi kujua kwamba anafahamika pia kwa jina la Scorpion.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mr. Chuz alisema kwamba yeye na wasanii wengine wote aliokuwa akifanya kao kazi, walikuwa wakimtambua kwa jina la utani la Sam Jet ambalo alipewa kutokana na aina ya upiganaji wake, ambao kuna muda alikuwa akijirusha na kupaa kama ndege.

NI KWELI ALIKUWA MLINZI WA KIMBOKA?

Kimboka ni baa maarufu iliyopo eneo la Buguruni Sheli. Muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo, yalisambaa madai mitaani kwamba Scorpion, alikuwa mlinzi (baunsa) katika baa hiyo na alikuwa akitumainiwa sana kuwadhibiti vibaka na wahalifu katika eneo hilo.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hilo katika baa hiyo, umebaini kwamba mtuhumiwa hajawahi kufanya kazi kwenye baa hiyo wala wahudumu na wafanyakazi wengine katika baa hiyo, wa zamani na wa sasa hawamjui.

Kwa nyakati tofauti, wahudumu na wafanyakazi wa baa hiyo walioomba hifadhi ya majina yao, walisema kwamba baa hiyo huwa haina ‘baunsa’ na shughuli za ulinzi huwa zinafanywa na ‘mmasai’ anayetumia kirungu na sime.

NI MKAZI WA WAPI?

Muda mfupi baada ya tukio la Scorpion kumjeruhi Said na kumtoboa macho, watu mbalimbali waliohojiwa, walidai kwamba mtuhumiwa huyo ni mkazi wa Buguruni kwa Mnyamani na kwamba ni maarufu sana maeneo hayo, kwamba hakuna mtu ambaye alikuwa hamjui.

Baadaye baadhi ya vyombo vya habari vikaripoti kwamba Scorpion alikuwa mkazi wa Yombo na vingine vikisema ni mkazi wa Tabata. Hata hivyo, swali la makazi sahihi ya mtuhumiwa huyo, limeendelea kuwa tata kwani imebainika kwamba si mkazi wa Buguruni, Yombo wala Tabata.

“Kiukweli hata hafamiki makazi yake halisi ni wapi ila hakai Buguruni, Yombo wala Tabata, hata watu wake wa karibu ukiwauliza, hakuna anayejua anaishi wapi,” kilisema chanzo chetu, maelezo ambayo yalipewa nguvu na mwalimu wake, Kaizile ambaye alisema licha ya kuwa naye karibu kwa kipindi kirefu, hakuwa anajua anakoishi.

NDIYE SCORPION WA BUGURUNI?

Uwazi halikuishia hapo, katika kuchimbachimba kwake, lilifanikiwa kupata maelezo juu ya mtu mwingine ambaye awali, watu walikuwa wakimchanganya kwamba ndiye mtuhumiwa wa tukio hilo, ambaye anafahamika zaidi Buguruni nzima kwa jina la Scorpion.

Gazeti hili lilifunga safari mpaka Buguruni ambako kwa msaada wa vyanzo vyetu, lilifanikiwa kukutana uso kwa uso na Scorpion wa Buguruni, ambaye cha kushangaza, ilibainika kwamba ni muumini safi wa dini ya Kiislam (ustaadh) na hakuwa akihusika kwa chochote na tukio hilo wala matukio mengine ya uhalifu.

Katika mahojiano naye, Scorpion wa Buguruni alionesha kushtushwa na taarifa ya jina lake kuhusishwa na uhalifu, akaendelea kueleza kwamba Buguruni nzima yeye ndiye anayefahamika kwa jina la Scorpion, haelewi huyo mwingine ni nani, anatokea wapi na kwa nini anajihusisha na uhalifu.

HANA REKODI YA UHALIFU

Baada ya tukio hilo, watu mbalimbali walikuja na shuhuda za matukio mengi ya ukatili yaliyokuwa yakifanywa na Scorpion, wengine wakisema ni kibaka mzoefu anayepora na kuua watu, wengine wakimtetea na kusema kwamba hakuwa kibaka bali muuaji wa vibaka ambaye ameshafanya matukio mbalimbali ya mauaji na ripoti zake zipo polisi.

Wikiendi iliyopita, Uwazi liliwasiliana na …………… wa Polisi ambaye alipoulizwa kama mtuhumiwa Scorpion ana rekodi zozote za matukio ya uhalifu, alijibu kwamba kumbukumbu za kipolisi hazioneshi kwamba amewahi kufanya kosa lingine lolote zaidi ya hilo la Said.

AMEOA, HAJAOA?

Miongoni mwa maswali mengine tata kuhusu mtuhumiwa huyo, lilikuwa ni kama ameoa au anaishi mwenyewe ambapo kila mtu alikuwa akizungumza lake. Lakini baada ya uchunguzi wa Uwazi, imebainika kwamba Scorpion amewahi kuoa lakini baadaye akaachana na mkewe, kwa hiyo mpaka tukio hilo linatokea, alikuwa akiishi mwenyewe.

Melezo hayo yalipewa nguvu na Mr. Chuz ambaye alithibitisha kwamba Scorpion amewahi kuoa lakini ‘akazinguana’ na mkewe na kuachana naye.

TAARIFA ZAKE NYINGINE

Taarifa zaidi zinadai kuwa mbali na kuwa msanii wa Bongo Movie, Scorpion amewahi kushiriki shindalo la kutunisha misuli jijini Dar es Salaam ‘Dume Challenge’ na kuibuka na kitita cha shilingi milioni ishirini.

Imeandikwa na Hashim Aziz, Gabriel Ng’osha na Leonard Msigwa.

Comments are closed.