The House of Favourite Newspapers

Matatizo Ya Moyo Yanasababisha Vifo

NI matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wa safu hii.

Leo tutajadili kwa kina matatizo ya moyo, ugonjwa ambao ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kuua watu duniani.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 12.5 miongoni mwa 32 milioni wanaopatwa na matatizo au mshituko wa moyo hufariki duniani kote.

Nchini Marekani pekee watu laki nne (400,000) na watu elfu 60 (60,000), hufariki dunia kutokana na ugonjwa huo kila mwaka ambapo ugonjwa huu huua wanawake zaidi kuliko wanaume kwenye nchi hiyo.

Ni mengi tuliyowaandalia katika safu hii na ni matumaini yangu kuwa yatakuwa yenye faida katika kutunza na kuimarisha afya zetu.

 

Dk. Godfrey Chale ataeleza kwa kirefu kuhusu tatizo hili na hapa anasema mshituko wa moyo hutokea wakati mtiririko wa damu yenye oksijeni unapozuiwa kwa ghafla katika misuli ya moyo.

Iwapo mzunguko wa damu hautaendelea haraka, kitendo hicho huifanya misuli ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na kuhatarisha maisha ya mwathirika.

 

Mshituko wa moyo kwa lugha ya tiba unajulikana kama ‘Myocardial Infarction’ inayomaanisha “Myo”.. muscles au msuli, ‘cardio’…. Heart au moyo na “infarct”….kufa kwa tishu kutokana na kukosa oksijeni.

Kama vilivyo viungo vingine mwilini hasa misuli, moyo nao huhitajia damu. Bila damu seli za moyo hudhoofika jambo ambalo husababisha mtu kuhisi maumivu.

 

Mshituko wa moyo hutokea pale mshipa mmoja wa damu au zaidi inaposhindwa kusafirisha damu yenye oksijeni katika moyo, kutokana na kuziba mishipa hiyo.

 

Mishipa ya damu inaweza kuziba kwa sababu tofauti kama vile, kuta za mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo (coronary arteries) kuwa nene, chembechembe za mafuta kujikusanya katika mishipa ya damu, kudhoofika na kukonda mishipa ya damu, mishipa ya damu inaposinjaa na kushikana au spasm na kujitokeza donge la damu katika mishipa ya damu.

Mshituko wa moyo mara nyingi husababishwa na ugonjwa wa moyo wa mishipa ya damu au Coronary Heart Disease (CHD).

 

Hii ni hali ambayo ndani ya mishipa ya damu hutokea kitu kiitwacho ‘plaque’ na kuzuia damu isiweze kupita katika mishipa ya damu, ambayo ni matokeo ya muda mrefu.

Lakini ni wakati gani mtu hukabiliwa na hatari ya kupata mshituko wa moyo?

Ni pale umri wa mtu unapoongezeka na kuwa mzee, mtu anapokuwa na unene wa kupindukia, kuvuta sigara, kuwa na shinikizo la damu au High Blood Pressure.

Kuishi bila kuwa na harakati na Mambo mengine yanayochangia kupata mshituko wa moyo ni baadhi ya magonjwa ya moyo, kufanyiwa operesheni ya moyo, kuwa na ndugu katika familia ambao wana matatizo ya moyo na jinsia ya kiume.

 

Uvutaji sigara husababisha mshituko wa moyo unaotokana na kuziba mishipa ya damu kwa asilimia 36, ambapo unene husababisha ugonjwa huo kwa asilimia 20.

Kukaa bila kujishughulisha au kufanya mazoezi husababisha mshituko wa moyo kwa asilimia 7 hadi 12.

Pia wanaume wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo zaidi kuliko wanawake katika kipindi chote cha maisha hasa kabla ya wanawake hawajafikia wakati wa kukatika hedhi.

 

Lakini kwa ujumla kwa kuwa wanawake huishi miaka mingi kuliko wanaume, magonjwa mengine ya moyo husababisha vifo vya wanawake uzeeni zaidi kuliko wanaume.

DALILI ZA MSHITUKO WA MOYO

Dk. Marise Richard yeye anazungumzia dalili za mshituko wa moyo. Anasema baadhi ya wakati mshituko wa moyo hutokea kwa dalili zilizo wazi na kwa haraka sana.

Lakini mara nyingi mshituko wa moyo hutokea polepole huku mtu akipata maumivu ya wastani na kutojisikia vyema.

Mara nyingi watu wanaopatwa na hali kama hiyo huwa hawana uhakika na kile kinachotokea na husubiri kwa muda mrefu kabla ya kuomba msaada au kumuona daktari.

Zifuatazo ni dalili ambazo hutokea pale mtu anapopatwa na mshituko wa moyo. Mosi; maumivu katika kifua.

 

Mara nyingi mtu anapopatwa na mshituko wa moyo huhisi maumivu sehemu za kifua hasa sehemu za katikati ya kifua ambayo huisha baada ya dakika kadhaa au mara nyingine maumivu hayo huisha na kurudi tena.

Mtu huhisi kana kwamba kifua kinambana, kimejaa na kinauma. Pili, maumivu katika sehemu za juu za kiwiliwili.

Mtu huhisi maumivu sehemu za mikono, mgongo, shingo, taya na tumbo. Tatu, kukosa pumzi au kushindwa kupumua.

 

Hali hii huweza kutokea ikichanganyika na maumivu ya kifua au bila maumivu hayo.

Dalili nyinginezo ni pamoja na kutoka kijasho chembemba (cha baridi), kujisikia kichefuchefu pamoja na kichwa kuwa chepesi na kizunguzungu.

 

Moyo kwenda mbio au mara nyingine mapigo ya moyo kwenda kasi zaidi kuliko kawaida.

Unashauriwa iwapo utajisikia mumivu ya kifua, hasa pamoja na mchanganyiko wa moja ya dalili tulizozitaja, usisubiri na haraka mpigie simu daktari au wasiliana na kituo cha afya ili upatiwe msaada, au elekea haraka hospitali mwenyewe.

Muda unaofaa wa kutibiwa mshituko wa moyo ni saa moja tangu wakati wa kutokea hali hiyo.

Kutibiwa mapema dalili za mshituko wa moyo hupunguza hatari ya kuharibika seli za moyo.

Hata kama huna uhakika dalili unazohisi ni za mshituko wa moyo au la, ni bora umuone daktari na ufanyiwe uchunguzi.

 

Utafiti waliofanyiwa wanawake 515 ambao walipata mshituko wa moyo umeonyesha kuwa, wengi wao waliripotiwa kuwa na dalili za kujihisi kuchoka, kutolala vyema, kushindwa kupumua, kujisikia maumivu baada ya kula na wasiwasi.

Asilimia 70 ya wanawake hao walihisi dalili zaidi ya moja kabla ya kupatwa na mshituko wa moyo.

Karibu theluthi moja ya kesi za ugonjwa wa mshtuko wa moyo hutokea kimya kimya, bila maumivu ya kifua wala dalili nyinginezo.

Kesi kama hizo hugunduliwa baadaye katika vipimo. Kesi kama hizo hutokea zaidi kwa wazee, wagonjwa wa kisukari na baada ya kuunganishwa moyo (heart transplant).

 

VIPIMO VYA MOYO

Tuangalie vipimo vya mshituko wa moyo. Kwa kawaida madaktari hufahamu kuwa mtu amepatwa na mshituko wa moyo au anaelekea kupatwa na mshituko huo kutokana na dalili alizonazo na anavyojisikia.

Pia kwa kutegemea historia ya kifamilia na ya kitiba ya mgonjwa pamoja na vipimo.

Kipimo kikuu kinachotumika kupima iwapo mtu amepatwa na mshituko wa moyo ni EKG.

Hicho ni kipimo kinachoonyesha na kurekodi mwendo na harakati ya moyo.

Kipimo hicho huonesha moyo unakwenda kwa kasi kiasi gani, mapigo ya moyo na mdundo wake.

Kwa hakika kipimo cha EKG huonyesha dalili za kuharibika moyo kutokana na matatizo ya mishipa ya moyo ya ugonjwa wa coronary heart disease na pia dalili za mshituko wa moyo uliotokea huko nyuma na unaotokea hivi sasa

Comments are closed.