The House of Favourite Newspapers

Mateso Ya Binti Huyu Usisikie!

AMA kweli hujafa hujaumbika! Ni maneno yanayoweza kukutoka utakapomaliza kusoma habari hii juu ya mateso anayopitia binti Fatuma Ally (14), mkazi wa Ukonga jijini Dar.

 

Fatuma amekumbwa na ugonjwa wa kichwa kujaa maji na pia hasikii wala haoni.

Akizungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda, mama mzazi wa Fatuma, Hilda Tulo anasema alimzaa Fatuma akiwa mzima kabisa, lakini alipofikisha umri wa mwaka mmoja alikwenda nyumbani kwao Tanga.

 

Anasema akiwa huko, Fatuma aliugua kifua na kumpeleka hospitalini ambapo alichomwa sindano.

“Mtoto alibanwa na kifua ikabidi nimpeleke hospitali, wakamchoma sindano, lakini tangu achome hiyo sindano, akawa hatembei tena vizuri maana alishaanza kuchanganya, nikaona labda ni kawaida.

 

“Lakini kadiri siku zilivyosoga ndivyo nilivyokuwa nikiona hali yake inazidi kuwa mbaya, hivyo nikarudi Dar na kumpeleka Hospitali ya Amana,” anasema mama Fatuma.

Aliendelea kusema baada ya kumpeleka Amana, aliambiwa ampeleke Hospitali ya CCBRT ambako walimpima na kugundua kuwa ana maji kichwani, hivyo wakamfanyia upasuaji kuyaondoa.

 

“CCBRT walimfanyia upasuaji, wakawa wamemtoa maji kichwani, kidogo akawa anaendelea vizuri na hapo alifanyiwa akiwa na miaka miwili, lakini alipofikisha miaka mitano, akaanza kusumbua kichwa kinamuuma huku akisema haoni vizuri.

 

“Nakumbuka kuna siku hatukulala usiku, alikuwa analalamika kichwa kinamuuma hivyo ilibidi asubuhi tuamkie Muhimbili,” anasema mama Fatuma.

Anasema walipofika Muhimbili, alipimwa na kugundulika kuwa ana maji tena kichwani, ndipo akafanyiwa upasuaji na kuyatoa, wakati huo macho yakapoteza kabisa muelekeo wa kuona.

 

“Kilichoniuma ni baada ya kuangalia uwezo wa kuona wa mwanangu, nikaambiwa haoni kabisa, niliumia sana, nikiwa sijakaa sawa, mtoto akapata tena tatizo la kutokusikia na walipomchunguza waligundua kuna mshipa ulipasuka, hivyo damu ikawa inasambaa hovyo. Ikabidi wamfanyie upasuaji tena wa kuondoa ile damu,” anasema.

 

Baada ya kufanyiwa upasuaji huo, usaha mwingi ukawa unatoka masikioni hasa wakati akiwa anacheka, kulia hata kulala. Hivyo kila baada ya muda walikuwa wakiufumua ule mshono na kusafisha na mwisho wakatoa mfupa uliokuwa umeoza kwa sababu ya usaha.

 

“Mwanangu alishafanyiwa upasuaji wa kichwa zaidi hata ya mara kumi kutokana na tatizo hilo la kutoka usaha, lakini tangu walipotoa ule mfupa uliooza, kuna afadhali kidogo na walisema nisubiri watamuwekea wa bandia.

 

“Kinachoniuma baba wa mtoto alinikimbia pamoja na ndugu zake wakidai kwenye ukoo wao hakuna tatizo hilo, hivyo nijue kwa kumpeleka. Nateseka na mtoto wangu, sina mbele wala nyuma, biashara zangu zote zimeisha kwa ajili ya kumtibu mwanangu, naomba Watanzania wenzangu wanisaidie ili mwanangu aweze kupata matibabu,” alisema mama huyo.

 

Kama umeguswa na tatizo la mtoto huyu na una chochote cha kumsaidia, unaweza kuwasiliana na mama yake kwa namba; 0715949778 na Mungu akubariki.

Comments are closed.