The House of Favourite Newspapers

Matibabu ya (HRT) Baada ya Kukoma Hedhi Kuuzwa Madukani Nchini Uingereza

0
Dawa ya kusaidia wanawake imepatikana

WANAWAKE wanaopata ukavu sehemu za viungo vya uzazi kutokana na kukoma hedhi sasa wanaweza kununua dawa madukani nchini Uingereza.

 

Vidonge vya Estradiol, vilivyouzwa chini ya jina la chapa Gina10, vilitolewa hapo awali kwa agizo la daktari tu.

 

Zitapatikana kwa wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 50 ambao hawajapata hedhi kwa zaidi ya mwaka mmoja, kama sehemu ya matibabu ya tiba ya uingizwaji wa homoni (HRT).

 

Wafamasia wamepewa mafunzo ya kutambua nani anahitaji vidonge hivyo.

 

Wakala wa Udhibiti wa Dawa na Bidhaa za Afya (MHRA) ulifanya uamuzi huo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufanya matibabu ya watu waliokoma hedhi kupatikana kwa urahisi zaidi kwa wanawake.

 

Vidonge vya Estradiol hutibu dalili za uke zinazosababishwa na ukosefu wa estrojeni, kama vile ukavu, uchungu, kuwasha, kuungua na kukosa raha kwenye tendo la ndoa.

Bidhaa hiyo huingizwa ndani ya uke badala ya kumezwa mdomoni.

 

Afisa Mkuu wa huduma ya afya ya MHRA Dkt Laura Squire aliita hatua hiyo “uainishaji upya wa kihistoria kwa mamilioni ya wanawake nchini Uingereza”.

 

“Katika kufikia uamuzi huu, tumeona uungwaji mkono chanya kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo wanawake wengi wenye umri wa miaka 50 na kuendelea ambao wanaweza kunufaika na uamuzi huu,” alisema.

 

MHRA inatumai hatua hiyo itaondoa shinikizo kwa huduma za mstari wa mbele za NHS na kuwapa wanawake uhuru zaidi katika kuchagua matibabu ambayo yanawafaa.

 

Dk Paula Briggs, mshauri wa afya ya kujamiiana na uzazi katika Hospitali ya Wanawake ya Liverpool, alisema 50-80% ya wanawake wanaopitia kipindi cha kukoma hedhi walipata ukavu wa sehemu za viungo vya uzazi.

 

“Hata hivyo inaweza kutibiwa kwa urahisi. Wanawake wengi wanaweza kutumia matibabu haya mapya na wanapaswa kutolewa kwa utaratibu,” alisema.

 

Imeandikwa na Peter Nnally kwa msaada wa mitandao.

Leave A Reply