The House of Favourite Newspapers

Mbowe: Siendi Polisi kwa Wito wa Makonda

DODOMA: Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hana mamlaka ya kumuita kwenda Kituo cha Polisi.

Mbowe ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma kufuatia kutajwa katika orodha ya watuhumiwa 65 wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kutakiwa kufika Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam leo saa tano asubuhi.

Mbowe amekanusha vikali tuhuma hizo za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kusema kuwa anachokifanya RC Makonda ni kuwaepusha watuhumiwa wa kweli wa dawa za kulevya na mikononi mwa sheria.

Aidha, Mbowe amesema kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi muda wowote endapo njia sahihi zitakapofuatwa. Pia amesema atamfungulia mashtaka RC Paul Makonda kwa kumchafulia jina lake kufuatia kumtuhumu kwa biashara ya dawa za kulevya.

Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni amesema kuwa wao hawana ugomvi wowote na Jamhuri bali Paul Makonda binafsi.

Wakati huo huo, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa jimbo la Hai,  Freeman Mbowe amekutana na kufanya mazungumzo na Wabunge kutoka Bunge la Ulaya, David Martin, Gerrard Quille, Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania, Roeland Van De Beer  na Waziri Kivuli wa Mambo  ya Nje, Afrika Mashariki na Kikanda,Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, mjini Dodoma leo Ijumaa 10/02/2017.

Comments are closed.