The House of Favourite Newspapers

Mechi Nne za Ubingwa Yanga

Kikosi cha timu ya Yanga

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera amewaambia Simba kwamba kama kikosi chake kikiendelea na moto kama wa juzi Jumanne dhidi ya Mwadui ndani ya mechi nne waandike maumivu.

 

Zahera ambaye ana uraia wa Ufaransa na DR Congo, alisema kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake kwenye kipindi cha pili katika mechi dhidi ya Mwadui na kushinda mabao 3-1 ni cha kuvutia.

 

“Wakati ligi ilikuwa imesimama tulifanya kazi kubwa sana na mazoezi ya nguvu sana ili kujiweka fiti, nadhani tukiendelea na kasi hii kwa mechi nne mfululizo itakuwa shida sana kutukuta,” alisema Zahera ambaye ni Kocha Msaidizi wa DR Congo.

 

“Programu ambayo wachezaji wangu wameipata imewasaidia sana tofauti na mwanzo ambapo hatukuwa na maandalizi ya maana, tulijiandaa wiki mbili tu kabla ya ligi kuanza. “Wakati ligi ilisimama juzi tulifanya programu moja ya nguvu ya kucheza mechi kumi. Ndani ya hizo mechi kumi timu itakuwa na fiziki kubwa sana na itakuwa fiti sana.

 

“Kwenye mechi ya Mwadui kipindi cha kwanza miguu ilikuwa mizito kutokana na aina ya mazoezi tuliyofanya, yalikuwa magumu sana. Lakini kipindi cha pili ilifunguka ndiyo maana wakacheza soka safi ambalo nadhani wakiendelea nalo ndani ya mechi nne mfululizo hakuna wa kutushika,” alisema Kocha huyo anayeishi kwenye ufukwe wa Kawe Jijini Dar es Salaam.

MAKAMBO NDANI

Straika wa Yanga, Heritier Makambo alitua jana usiku na kuwahakikishia mashabiki wa klabu hiyo kwamba hakutoroka kama inavyozushwa bali alipewa ruhusa na uongozi na Zahera mwenyewe. “Nipo Yanga, watu wanaongea kwamba mimi nimeondoka …nimekimbia.

 

Siyo kweli, mimi sikutoroka. Nilikuwa na ruhusa maalum kutoka kwa kocha na viongozi wanajua. “Nilikuwa na matatizo yangu ya kifamilia, nimerudi kazini kumaliza kazi. Nipo sawa, nimerudi kufanya kazi ya uhakika. Mungu atusaidie, tufanya kazi,” alisisitiza Makambo ambaye ana mabao 11 kwenye msimamo wa wafungaji wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

ZAHERA KIBURI
Zahera amefunguka kwamba ndani ya kikosi hicho hakuna hata nyota mmoja ambaye anamsumbua kichwa endapo atamkosa kutokana na sababu yoyote ile. “Siyo Makambo tu ambaye hakuwepo kwenye mechi yetu iliyopita bali hakuna mchezaji yeyote ambaye ananiumiza kichwa endapo ikitokea kwamba tumemkosa.

 

“Kama unakumbuka siyo yeye tu tulimkosa Kelvin Yondani katika mechi saba pia Ibrahim Ajibu kwenye mechi tano lakini mara zote hizo tulishinda michezo yetu. “Niseme tu kwamba hapa hakuna nyota ambaye ananiumiza kichwa endapo ikitokea kwamba tumemkosa kwenye mechi hata moja,” alisema Zahera ambaye huwapa ofa ya mshiko wachezaji wake mara mojamoja.

Comments are closed.