The House of Favourite Newspapers

MGOMBA HAUCHANJWI KUNI

TEENAA na mtani-koma mwaka huu kama hujaishi mbona utaishi tu kwani ndiyo maisha yetu ya mjini, unachuma tembele huku umeinama, unachuma kisamvu huku umesimama, uongo nyonyo?  Kama nakuona ulivyo na kimuhemuhe cha kutaka kujua Anti Naa leo amekuja na nini? Hebu tulia kama pipa lililokosa mfuniko! Halooo eeeehhh mwenziyo nina utamu wa kuku natafunwa hadi mifupa, kila Jumatano nipo kukupa burudani kama siyo elimu!

Shoga baada ya kukupa  udambwidambwi, tuelekee kwenye kileeee kilichonileta, kilichonisukuma hadi nije nishee na wewe, maana waswahili wenzangu wanasemaaa hata saa iliyosimama kuna wakati inasema ukweli, upo?

Leo nitaongea na hawaaa wamama ambao wanaona maisha kwao bado yapoyapo, utakuta mama mtu mzima miaka arobaini anaenda hamsini tena anakaribia kuitwa bibi lakini ndiyo kwanza anataka kujifanya kama kibinti cha miaka ishirini, klabu za usiku yumo, kuolewa hataki, kuzaa hataki akifikisha miaka hamsini na kitu ndiyo anaanza kutafuta wa kuolewa naye na hapohapo anataka kuwa na mtoto, aliyekwambia mgomba huwa unachanjwa kuni nani? Shuuutuuuu!

Ulikuwa na utamu wa samaki sasa hivi umebaki miba ndiyo unashtuka? Heee heeeiyaaaaaa, unalooo mbooona! Wakati mwingine huwa najiuliza sana, sawa una miaka arobaini naa ndiyo unashtuka kuwa  unataka kuzaa, baada ya miaka 15 au 20 huyo mtoto unataka akuite nani kama siyo bibi?

Badilika shoga, muda haurudi nyuma, usitake kuona ujana kama ndala ambayo thamani yake mwisho chooni ukirudi ndani inaishia mlangoni! Mwenzako sina roho mbaya maishani mwangu, nitakufa kama muwa na utamu wangu na kama ulikuwa hujui, maneno yangu kuntu yaweza kukuelimisha kuliko ya punguwani yaweza kukudhalilisha, upo nyonyo?

Kama ukichelewa vyote angalau basi isivuke miaka arobaini yaani iwe chini ya thelathini, hata ukizaa au kuolewa utaona thamani ya ndoa na kufurahia ujana wenu kuliko kufurahia mkiwa wazee mkaishia kupata watoto wawili na wote wakawaita babu na bibi!

Achana na maneno ya washamba waliokuja mjini na gari la samaki kutwa kunuka shombo! Wao kazi yao kukudanganya na kukufanya ujione umri bado upo uendelee kula bata, shtuka shoga ukiwa bado mbichi utafute mbichi mwenzako muanze maisha haloooo eeh!

Kwa leo sitaki kuongea saaana, tukutane tena wiki ijayo, ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu!

Comments are closed.