The House of Favourite Newspapers

Mitandao Ya Kijamii Inaweza Kukupa Mume, Mke Mwema?

0

MITANDAO ya kijamii imerahisisha sana mambo. Wapo wanaoitumia vizuri na kuweza kufanikisha mambo mbalimbali ikiwemo biashara na fursa mbalimbali ikiwemo ajira na mambo mengine kadha wa kadha. Katika ulimwengu wa wapendanao, wapo pia wanaoitumia vizuri na kujikuta wakifikia hatua ya kufunga ndoa. Urafiki unaanzia kwenye mitandao ya kijamii, unakua na baadaye unaleta matunda mazuri, ndoa. Kabla ya ujio wa mitandao hii, mambo yalikuwa magumu kidogo.

Ilikuwa ikimchukua muda mrefu sana mwanaume kukutana na mwanamke kutokana na mazingira na umbali. Kulikuwa na shughuli fulani hadi mwanaume aweze kumfikia mwanamke. Hiyo ilikuwa inaleta heshima fulani hata katika suala zima la maadili.

Kulikuwa na nidhamu ya hali ya juu, mwanaume alikuwa anamuona mwanamke, anamchunguza kwa muda kuweza kujiridhisha tabia zake na mambo mengine kabla ya kufikia hatua ya kumtongoza. Vivyo hivyo kwa mwanamke. Anajiridhisha kwanza kwa mazingira anayoishi mwenzi wake, familia anayotoka na kumsoma tabia ndipo aamue kuingia kwenye uhusiano.

Tofauti na zamani, mitandao hii imeleta urahisi wa kukutana, suala la kuchunguza limepewa kisogo. Watu wamekuwa wakiigiza. Wanaweka picha makusudi katika mitandao hiyo kutafuta biashara. Wanaume wanafanya hivyo lakini wanawake ndio wanaongoza zaidi. Wanaume wanaweka picha, wanawake wakivutiwa nazo basi wanaomba mawasiliano hapohapo na biashara inakuwa imekwisha.

Mwanaume ataomba atumiwe picha za kuthaminisha kupitia mtandao wa WhatsApp na baada ya muda wanakutana. Maadili yale na staha za kike siku hizi zimeharibiwa na mitandao ya kijamii. Mwanamke akiingia tu ‘online’ na kukutana na mwanaume, hana cha kusubiri. Anaanza kumtongoza. Anajenga tu hisia kwamba yule anayemuona ni sahihi. Anaamini kwamba atakuwa tu hana mtu.

Anajirahisisha na kuanza kuomba urafiki. Mwanaume naye bila hiyana anamkubalia. Anajua tu atamtumia halafu biashara inaishia hapo. Hapo hakuna maelezo marefu. Mwanamke anajua kinachofuata ni nini. Kukaa baa, kununuliwa vinywaji kisha safari ya gesti inaiva.

Hakuna muda wa kusubiri kuchunguzana. Kizazi kimefikia huko, hakuna ambaye anaweka nguvu kubwa katika pendo. Wanasema ni kumalizana leo leo tu. Nipe fedha, tutumie halafu tumalizane. Pamoja na kwamba mitandao hiyohiyo inaweza kukupa mke au mume mwema lakini kimsingi ni kwa asilimia chache sana kutokana na mmomonyoko wa maadili uliochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Laiti ingetumika vizuri, ungekuwa ni uwanja mzuri wa watu kuweza kukutana na wachumba wa uhakika na baadaye kuingia hata kwenye ndoa. Maadili yameshushwa na utandawazi huo. Matokeo yake kila unayemuona yupo humo, ni kama vile wote wamefundishwa na mwalimu mmoja.

JIFUNZE Asilimia kubwa ya watu wa mitandaoni si waaminifu. Wameondoa ile dhana halisi ya urafiki hivyo ni vyema ukawa makini. Unaweza kuutumia mtandao wa kijamii kupata rafiki lakini ichukulie kama hatua ya kwanza lakini hatua ya pili ni kumchunguza. Chukua muda wa kumchunguza.

Usikubali kirahisi kuingia kwenye mtego na mwenzako akawa amekutumia na kufanikisha lengo lake. Msome huyo mtu amekupenda kutoka moyoni au amekutamani kutokana na picha za mitandaoni? Ana tabia njema? Si mhuni kama walivyo wahuni wengi wanaopatikana katika mitandao ya kijamii? Ana hofu ya Mungu? Amekulia katika mazingira gani? Majibu ya maswali hayo yote unaweza kuyapata pale tu utakapo muweka karibu na kumchunguza kabla ya kuamua kuanzisha naye safari ya maisha ya uhusiano.

Mwenye nia ovu, hana uvumilivu wa kuchunguzwa muda mrefu. Utambaini tu kwa matendo yake. Achana naye kabla hujazama penzini na utapata mwenzi sahihi wa maisha, iwe ni kwa njia ya mtandao wa kijamii au hata kwa kukutana na mtu ana kwa ana.

WEKA AKILINI Mitandao ina kiwango kikubwa cha matapeli wa mapenzi hivyo ni vyema kuanzisha uhusiano na mtu unayemfahamu vizuri ambaye mmefahamiana kwa njia ya kawaida tofauti na mitandao ya kijamii. Mitandao hiyo ibaki kuwa sehemu ya biashara nyingine na si mapenzi. Tukutane wiki ijayo.

Leave A Reply