The House of Favourite Newspapers

Mambo ya Kuzingatia Kabla Hujaamua Kumtoa ‘out’ Umpendaye

Shukrani za kipekee zimuendee Mungu kwa kutuwezesha kuiona salama siku ya leo, ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko vizuri na unaendelea kulisongesha mbele gurudumu la maendeleo, leo utakuwa nami Baby Madaha.

Wataalamu wengi wa masuala ya mapenzi, wamekuwa wakisisitiza juu ya umuhimu wa kumtoa ‘out’ umpendaye katika kuboresha upendo kati yenu. Hata hivyo, ni wachache wanaojua nini wanatakiwa kufanya na nini hawatakiwi kufanya wanapotoka na wapenzi wao.

Ni matumaini yangu kwamba makala haya yatakusaidia kuelewa maandalizi muhimu na mambo ambayo hutakiwi kuyafanya mnapotoka na umpendaye.

Unapopanga kutoka na umpendaye, ni vizuri kufanya maandalizi ya kutosha ya vitu vyote muhimu ili siku ikifika, isionekane umekurupuka. Ni vizuri kufanya maandalizi ya sehemu unayotaka kumpeleka mwenzi wako na kuhakikisha ina utulivu wa kutosha na usalama.

Baada ya kuwa na uhakika na sehemu mtakayoenda, ni vizuri kujiandaa wewe binafsi. Andaa nguo safi, fanya usafi wa mwili ikiwa ni pamoja na kuoga vizuri na kupiga mswaki kwani mkiwa out, lazima mtasogeleana na mwenzi wako hivyo kama unanuka mdomo au jasho, unaweza kuwa kikwazo kwa mwenzi wako.

Hata kama hatakwambia, hatafurahia kuwa na wewe karibu. Unaweza pia kujipulizia marashi mazuri yatakayoongeza bashasha.

Baada ya maandalizi ya awali kuwa yamekamilika, jitahidi kuwahi kabla ya muda mliokubaliana. Akifika na kukukuta tayari umeshafika na kumsubiri, ataona umempa kipaumbele, jambo litakalomfurahisha. Mpokee kwa uchangamfu, inuka, muoneshe sehemu ya kukaa na akishakaa na kutulia, na wewe kaa kisha muulize kitu atakachokipendelea.

Anzisha mazungumzo ya kawaida huku ukijitahidi kuwa na tabasamu kwenye uso wako kwani kuna usemi wa wahenga kwamba tabasamu ni kama uchawi wa kimapenzi, hata kama mwenzi wako ana hofu ndani ya moyo wake, akikuona umetabasamu, atatulia na kufurahia kuwa pamoja na wewe.

Watu wengi huwa wanakosea jambo moja, unakuta bibi na bwana wametoka ‘out’ lakini kila mmoja yuko bize na simu yake. Mwanaume yuko bize kuchat WhatsApp au Facebook, mwanamke yuko bize Instagram au kutuma meseji za kawaida.

Nakushauri msomaji wangu usiwe na tabia kama hii kwani haileti picha nzuri. Ikiwezekana, zima kabisa simu yako au itoe mlio ili akili yako yote uielekeze kwa mwenzi wako. Utajisikiaje pale unapomwambia mwenzio kitu kizuri lakini kumbe wala hakusikilizi yuko bize na simu yake? Haileti picha nzuri.

Kama wewe ni mtumiaji wa kilevi, jizuie kunywa hadi kulewa wakati ukiwa kwenye mtoko na mwenzi wako. Kwa kawaida, mtu aliyelewa, hawezi kuzungumza kwa busara, anaweza kufanya jambo lolote la aibu bila kujijua na hawezi kuwa makini katika mazungumzo. Epuka kulewa ukiwa out na mwenzi wako.

Badala ya wewe kuwa mzungumzaji mkuu, washauri wa mambo ya mapenzi wanaeleza kwamba ni lazima uongozwe na busara katika kila unachokizungumza. Achana na habari za wapenzi wako waliopita, zungumza naye mambo mazuri ikiwemo mipango ya maisha ya baadaye na jitahidi kuwa msikilizaji kuliko mzungumzaji.

Ni matumaini yangu kwamba ukizingatia haya, utafanikiwa ‘kumroga’ mpenzi wako, ataendelea kukupenda na muda mwingi atakuwa akikufikiria wewe pamoja na kukumbuka mambo mazuri mliyoyafanya pamoja mkiwa out.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

JONAS MKUDE ATAMBULISHWA RASMI YANGA, APEWA JEZI NAMBA 20…

 

Comments are closed.