The House of Favourite Newspapers

LIVE: Mjadala Huru Kuhusu Mbinu Zinazotumiwa na Serikali Kutokomeza Viroba

LEO Machi 9, 2017 waandishi na wahariri wa Kampuni ya Global Publishers wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Eric Shigongo, wamefanya mjadala huru LIVE (Mubashara) kupitia Global TV Online na kuchangia mawazo kuhusu mbinu na njia ambazo serikali ingezitumia kutokomeza matumizi ya vifungashio vya plastiki kwa pombe kali maarufu kama viroba.

Mwandishi Gabriel Ng’osha akizungumza

Lengo la mjadala huo lilikuwa ni namna bora ambazo serikali inapaswa kuzitumia ili kukabiliana na jambo hilo bila kuwaathiri wananchi wake.

 

Philip Nkini akichangia mada

Akichangia katika mjadala huo,  Mharriri wa  Gazeti la  Championi, Philip Nkini alisema haya:

“Kwanza Serikali haikutoa  muda wa kutosha hadi kuwawekea zuio wauzaji wa pombe hizo na vifungashio vyake, hivyo serikali ilipaswa kukutana na wafanyabiashara na kuzungumza nao kabla ya kuweka zuio hilo. Kinachotakiwa kwa sasa, serikali ikae na wafanyabiashara iwape elimu kabla ya kuwazuia.”

Saleh Ally akichangia mada

Naye Mhariri Mtendaji, Saleh Ally alisema haya:

“Vifungashio vya viroba ni hatari kwa mazingira, pili ni hatari kwa afya. Namna ya kulifanya jambo lenyewe la kutokomeza viroba halijakaa sawa, serikali ingeanzia viwandani kwanza ndipo irudi kwa wafanyabiashara.

“Watendaji watumie njia zilizo sahihi. Kama leo wafanyabiashara wameanza kujiua sababu ya viroba… watajiua wangapi? Naiomba serikali yangu sikivu itumie njia sahihi kwenye suala hili kwani Tanzania haiwezi kuwepo bila wananchi.”

Mchangiaji mwingine ambaye ni Mhariri wa Gazeti la Risasi Jumatano, Ojuku Abraham akachangia kwa kusema:

“Tukumbuke kuwa serikali haijapiga marufuku pombe, imepiga marufuku vifungashio na haijaanza leo tangu mwaka 2013 ndipo ilitoa tamko hilo.

 

“Hata kama wakipewa muda bado tatizo litakuwa lile lile na utekelezaji hautofanyika, hivyo mimi niwaombe wananchi wenzangu, jambo linalopigwa marufuku na serikali sisi wananchi tuungane na tutekeleze.”

Naye Mhariri Kiongozi, Oscar Ndauka akachangia kwa kusema:

“Naishauri serikali iache kukurupuka. Kwanza ingeanzia viwandani polepole zile pombe zilizokuwa zikifungwa kwenye viroba zikawa zinafungwa kwenye chupa zinaingizwa sokoni huku ikiziba polepole mianya ya kutengeneza mifuko ya plastiki.. mwisho wa siku viroba vingepotea.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, Eric Shigongo akichukua pointi za wajumbe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, Eric Shigongo akiwa kama mjumbe kwenye mjadala huo akatoa maoni yake:

“Naomba nianze na kuipa pole familia na ndugu wa mfanyabiashara aliyejiua Dodoma. Kwa upande wa wafanyabiashara wenzangu niwasihi wasikate tamaa, tujiepushe na maamuzi magumu kama kujiua maana tutaziacha familia zetu kwenye wakati mgumu.

“Naomba pia niishauri serikali ihakikishe wananchi wake wako salama…. Sisi kama taifa lazima tujifunze mbinu za kuzuia mambo kadha wa kadha ndani ya nchi yetu.”

Comments are closed.