Mkuki Moyoni Mwangu – 67
ILIPOISHIA…Ili kuendelea kubaki na Catarina mama wa mtoto wake mtarajiwa, Jamal anaamua kumsaidia Kevin kwenda porini kumsaka Catarina ndani ya kichwa chake akifahamu jambo moja tu; kuhakikisha anamwacha mwanaume huyo hukohuko porini ambako asingetoka salama na lazima angekuwa chakula cha wanyama wakali.
Anarejea nyumbani na kukutana na mke wake baada ya maongezi mafupi Jamal anaingia bafuni kuoga na kupanda kitandani kupumzika, Catarina kwa kupitia dirishani anachungulia na kuona gari la mpenzi wake huyo ni chafu kupindukia uamuzi anaochukua ni kutoka nje na kuanza kuliosha.
Ghafla nyuma ya kiti cha dereva analiona begi anaamua kulichukua na kufungua ndani macho yake yanakutana na kitu kisicho cha kawaida, kitabu kidogo moyo wake unamtuma kukichukua na kukifungua, machozi ya uchungu yakimbubujika haamini alichokisoma ndani yake. Anarejea ndani kwa hasira anamtaka Jamal aamke ili amweleze ukweli ni wapi alipompeleka Kevin wake.
Jamal anashuka kitandani na kupiga magoti mbele ya Catarina, akilia kama mtoto mdogo, huku akisimulia mkasa mzima wa namna alivyokutana na Kevin ofisini kwake, akajitolea kumsaidia ingawa lengo lake halikuwa kufanya hivyo, bali alitaka kumwondoa duniani ili awaache wawili na mtoto wao atakayezaliwa waishi vizuri kwa raha mustarehe. Kwa saa mbili wote waliendelea kulia Catarina akimlaumu Jamal kwa kitendo chake cha kutoa uhai wa mtu asiye na hatia.
Je, nini kitaendelea? Catarina atamsamehe Jamal?
SONGA NAYO…
“
UMEKOSEA, umeniumiza, nilikuwa tayari kuishi na wewe maisha yangu yote, lakini kwa sababu umeua, upendo wangu umepungua, sina uhakika tena kama nitaweza kuishi na wewe siku zote za maisha yangu!”
“Nisamehe!”
“Nimekusamehe Jamal lakini…”
“Lakini nini tena mpenzi wangu, nilifanya kosa, niliamua kumpeleka Kevin porini ili aliwe na wanyama wakali ili kulinda penzi langu, moyo wangu unakupenda, wewe umekuwa mrithi wa Vivian, hakika sikuwa tayari kukuacha uondoke.”
“Najua unanipenda, nami nakupenda pia lakini kitendo ulichokifanya kimefanya nikuone mtu mbaya na katili kuliko wote niliowahi kukutana nao.”
Maneno hayo pekee yalikuwa ni kama mkuki ndani ya moyo wa Jamal, bila kusema kitu akainamisha kichwa chake chini na kuanza kulia, wakati huo hakuhitaji kitu kingine chochote zaidi ya kusikia kwamba Catarina alikuwa amemsamehe na maisha yaendelee kama ilivyokuwa mwanzo.
“Jamal!”
“Ndiyo.”
“Nitajitahidi kukupenda tena lakini si kama mwanzo, ni kweli hivi sasa mimi ni mjamzito mtoto aliyeko tumbo ni damu yako hana hatia pengine ningependa kumzaa akikua na kumwona baba yake lakini kwa sasa sina uhakika huo, umenibadilisha Jamal, umenitenda jambo baya kuliko, upande fulani sikulaumu kwa kilichotokea lakini upande mwingine nakulaumu umekuwa mnyama.”
“Catarina ninakusihi naomba unipende kwa nafasi nyingine, ishi na mimi, tupendane kama ilivyokuwa mwanzo, nitakuwa tayari kufanya chochote utakachoniambia ili mradi tu usiniache.”
“Nahitaji kufikiria upya, kwa leo sina jibu la kukupa,” alijibu Catarina na bila kuongea tena kitu chochote akapanda kitandani ambako aliendelea kumlilia Kevin.
Kazi ya Jamal ikawa moja tu, kumbembeleza mpenzi wake, alifanya kila alichoweza ili kurejesha furaha ya Catarina, kwa muda wa wiki nzima bado hali ilikuwa ileile ndani ya nyumba, mara kadhaa akirejea kazini na kukuta Catarina akilia na kuomboleza jambo lililozidi kumtia wasiwasi kutokana na hali yake ya ujauzito.
Alipotoka alirejea akiwa na zawadi mbalimbali ili tu kupata msamaha lakini bado Catarina hakuonyesha kukubaliana na chochote kile, hata alipoingia jikoni na kupika chakula kisha kumkaribisha na kumwomba ale bado hakupata ushirikiano wa aina yoyote, muda wote kwa Catarina ilikuwa ni kulia tu. Jamal akachanganyikiwa hakuelewa afanye kitu gani tena zaidi ili tu kurudisha furaha ya mwanamke aliyempenda kuliko wote.
“Nimejaribu kufanya kila kitu ili kurejesha furaha ya Catarina lakini nimekwama na inavyoonekana kama hali itaendelea hivi nitampoteza yeye pamoja na mtoto wangu, sitaki hili litokee, sitachoka kumwomba msamaha mwisho atanisamehe tu, kwani hana namna yoyote ile isipokuwa kuwa na mimi.” Aliwaza Jamal siku moja akirejea kutoka kazini. Alifika nyumbani na kuegesha gari lake, kwa muda aliendelea kubaki ndani yake akitafakari ni nini angefanya ili kurejesha penzi lililoanza kwenda mrama.
Baada ya muda Jamal aliamua kushuka na kutembea kuelekea ndani, moyoni mwake akiwa na hofu hakuelewa siku hiyo Catarina angekuwa na jambo gani jipya kwani kila siku iliyoitwa leo kulizuka jambo geni, kadri alivyozidi kupiga hatua kuuelekea mlango ndivyo mapigo yake ya moyo nayo yalivyozidi kuongezeka. Kifupi alimuogopa Catarina kupindukia.
Taratibu huku akionekana mwenye wasiwasi mwingi akausukuma mlango na kuingia ndani yake, macho yake yakazunguka huku na kule sebuleni bila kumwona Catarina, haraka akapiga hatua na kuzama chumbani, nako hakumkuta, Jamal akahisi kuchanganyikiwa.
“Catarina! Catarina! Catarina wangu!” Aliita lakini hakupata ushirikiano wowote, ukimya wa ajabu ukaifunika nyumba yake.
“Hawezi kuwa ameondoka,” alijisemea huku akitoka nje ya nyumba na kuzunguka huku na kule.
Ghafla macho yake yakatua kwenye moja ya msingi wa nyumba yake, alimwona mtu akiwa ameketi huku akiwa amejiinamia chini haraka akapiga hatua na kumfikia.
“Catarina! Catarina mpenzi wangu! Kimetokea nini?”
“Jamal!”
“Naam!”
“Unajua ninakupenda.”
“Ndiyo najua mpenzi wangu mimi pia ninakupenda sana.”
“Ahsante kwa kunipenda, uliokoa maisha yangu bila wewe nilishaliwa na wanyama wakali porini.”
“Najua!”
“Nimekusamehe kwa moyo wangu wote, kinachoniumiza hivi sasa ni namna Kevin wangu alivyokufa, hakuwa na hatia, lakini ninachotaka kukueleza hapa ni kwamba hata nikilia kwa miaka elfu kumi bado sitamwona tena Kevin maisha yangu yote yaliyobaki, jambo moja naomba nisikie kutoka kwao nahitaji upendo wa kweli ambao utanifanya nimsahau Kevin.”
“Nakuahidi mpenzi wangu, nitafanya kila liwezekanalo kukupa furaha si wewe tu hata mtoto wangu atakayezaliwa nitampenda kupindukia.”
“Pamoja na kukupa msamaha ni kweli kwamba nitamkumbuka Kevin siku zote si rahisi kumtoa moyoni mwangu ni mwanaume aliyenipenda kama ilivyo wewe, Mungu naomba umpokee kama atakuwa amekufa basi tukutane tena siku ya mwisho, umpumzishe mahali pema peponi, amekufa akijaribu kuutafuta ukweli wa mahali nilipo….” Aliongea Catarina na hakuweza kumalizia sentensi yake kwikwi ya kulia ikamkatamata.
Jasho jembamba likamtiririka Jamal, kitendo cha Catarina kumwambia kwamba amemsamehe kwa moyo wake wote, kwake ilikuwa kama ndoto alihisi yu usingizini na muda si mrefu angezinduka na kujikuta kitandani, taratibu akanyoosha mikono yake na kumkumbatia Catarina kisha kuachia mabusu mfululizo.
“Nitakupenda siku zote, niko tayari kulilinda penzi letu mpaka mwisho. Kwa mara nyingine tena mpenzi wangu naomba unisamehe…”
“Nimeshakusamehe tena kwa moyo wangu wote Mungu akusamehe pia na ninamwomba ampokee Kevin huko aliko,” aliongea Catarina taratibu Jamal akiwa amemshika mkono wakipiga hatua kuingia ndani ya nyumba yao.
“Ahsante,” alijibu Jamal akionyesha furaha ya ajabu.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

