The House of Favourite Newspapers

Mlemavu Adaiwa Kujinyonga

0

MLEMAVU wa miguu, Majami James (57), amepoteza maisha baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kamba ya katani kwenye mti, nyuma ya nyumba yake.

 

Ilidaiwa kuwa mwanaume huyo aliyekuwa akiishi katika Kijiji cha Kasahunga, Kata ya Neruma, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, alijinyonga kutokana na msongo wa mawazo.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tubishubwamu, alisema jana kuwa mlemavu huyo mjasiriamali alijinyonga saa 12 asubuhi kijijini hapo.

 

Kamanda Tubishubwamu alisema mwananchi huyo aliyekuwa na kibanda cha biashara, pia alikuwa fundi cherehani kijijini hapo.

 

Alisema siku moja kabla ya tukio hilo kulikuwa na kikao cha wanafamilia na wana ukoo kujadili mwenendo wa James kimaisha.

 

Kamanda Tubishubwamu alisema mwili wa James ulikutwa ukining’inia juu ya mti, nje kidogo ya nyumba yake.

 

Alisema wakati wakipekua kwenye mfuko wa nguo ya marehemu walikuta karatasi iliyokuwa na maandishi kwamba asisumbuliwe mtu yeyote kuhusu kifo chake, kwani ameamua kujitoa uhai wake yeye mwenyewe kutokana na msongo wa mawazo.

 

Kamanda Tubishubwamu alitoa wito kwa wananchi wamrudie Mungu na wanapopata changamoto zikiwemo za kimaisha waombe ushauri kwa wenzao na viongozi wa dini.

 

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospitali teule ya Halmashauri ya mji wa Bunda.

Leave A Reply