Mo Ajibu Mapigo, Aweka mil 120
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’ naye jana usiku alivamia kambi ya timu hiyo na kula chakula cha pamoja na wachezaji wake sambamba na kufanya kikao kizito na mastaa wake.
Hiyo yote katika kuleta hamasa ya mchezo wa Dar es Salaam Dabi utakaopigwa leo saa 11:00 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ili wapate matokeo mazuri ya ushindi. Katika mchezo huo, Yanga wataingia uwanjani wakiwa na pointi 23 wakiwa katika nafasi ya pili huku Simba wenyewe wakiwa na 19 ambao wanatakiwa kushinda ili wapunguze gepu la pointi dhidi ya wapinzani wao.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Mo alitarajiwa kukutana na kula chakula cha jioni cha pamoja na wachezaji kwenye Kambi ya timu hiyo, Ndege Beach nje kidogo ya Jiji la Dar. Mtoa taarifa huyo alisema kuwa hiyo ni kawaida ya bilionea huyo kukutana na wachezaji kufanya kikao siku moja kabla ya mchezo, lengo ni kuwapa hamasa na kufahamu umuhimu wa mchezo huo.
Aliongeza kuwa bilionea huyo tofauti na kupata chakula hicho cha jioni, alitarajiwa kutoa ahadi ya fedha ya Sh 120Mil kwa wachezaji wale watakaokuwepo kwenye sehemu ya wachezaji 11 watakaoanza na wale wa akiba pekee watakaoipa ushindi timu hiyo.
“Siyo mara ya kwanza kwa Mo kutoa ahadi ya fedha kwa wachezaji wake watakaocheza Dar es Salaam na kuipa matokeo mazuri ya ushindi, hivyo jana usiku alitarajiwa kukutana na wachezaji wote kwa ajili ya kufanya kikao.
“Kikao hicho, pia kiliwahusu benchi lote la ufundi katika kuelekea pambano hilo na kikubwa Mo alitoa ahadi ya fedha kwa wachezaji wake kama watafanikiwa kuifunga Yanga katika mchezo huo. “Ameweka kiasi cha Sh 120Mil kwa wachezaji wa kikosi cha kwanza na wale wa akiba, fedha hizo ameahidi kuzitoa mara baada ya mchezo huo kumalizika,” alisema mtoa taarifa huyo.
Gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa timu hiyo, Dk Arnold Kashembe kuzungumzia hilo, alisema: “Sisi kila mchezo tunatoa posho kwa wachezaji wetu ambayo ambayo tunaitoa pale tunapopata ushindi. “Tuliianza tangu msimu uliopita, hivyo siyo kitu kigeni kwetu na kuhusu kiwango cha fedha tulichoweka ni siri ya viongozi na wachezaji.”
Wilbert Molandi na Marco Mzumbe, Dar