Mo Aleta Kifaa Kipya Simba SC
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameleta kifaa kipya kutoka nje ya nchi kitakachotumika kuwapima wachezaji wao.
Hiyo yote katika kuhakikisha wanatengeneza fitinesi ya wachezaji wao wakiwa katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mo alisema kifaa hicho wamekabidhiwa viongozi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mbelgiji Sven Vandenbroeck na tayari kimeanza kufanya kazi.
Mo alisema kuwa kifaa hicho kinafanya kazi ya kupima oxygen, spidi ya mchezaji jinsi anavyojituma uwanjani katika mechi na mazoezi kuhakikisha anatengeneza fitinesi ya wachezaji wa timu hiyo.
“Niliahidi kuleta kifaa maalum kitakachopima oxygen, spidi na kujituma kwa kila mchezaji akiwa uwanjani, kifaa kina umuhimu mkubwa kwa wachezaji katika kutengeneza fitinesi zao.
“Kwani kama mchezaji hatakuwa hajitumi uwanjani, basi kutamrahisishia kocha kufahamu kasi yake na mchango wake anaoutoa akiwa anaipambania timu yake,” alisema MO.
WILBERT MOLANDI, Dar