The House of Favourite Newspapers

Mr Nice Awaponda Wanamuziki Wapenda Kiki

UNAPOZUNGUMZIA wanamuziki walioutoa mbali muziki wa Bongo Fleva huwezi kumuacha mkali wa miondoko ya Takeu, Lucas Mkenda ‘Mr Nice’.

Mr. Nice ni alama isiyofutika kwenye muziki Bongo kutokana na mchango aliouweka kwenye muziki huo ikiwemo kufanya ngoma kali kama vile Kikulacho, Fagilia na nyingine nyingi.

Hata hivyo baada ya kutikisa kwenye tasnia hiyo, Mr. Nice kwa sasa ni kama amepotea hivi, amekuwa akijaribu kufurukuta kurudi kwenye enzi zake bila mafanikio.

 

Gazeti hili lilimtafuta ili aweze kuzungumzia nini hasa kinamkwamisha kurudi kwenye ukali wa muziki aliokuwa nao zamani na kwa sasa muziki wake hasa anafanya akiwa wapi! Huyu hapa chini.

Risasi: Mambo Nice, hivi karibuni ulikuja na ujio wa Yaya lakini ni kama umebuma, tatizo nini?

Mr. Nice: Siyo hivyo, ngoma haijapata tu ‘air time’ kubwa kwenye redio, lakini klabu na sehemu nyingine inafanya vizuri.

 

Risasi: Sawa, je ni changamoto zipi ambazo umekuwa ukikumbana nazo, mpaka unashindwa kurudi kwenye levo zile za zamani?

Mr. Nice: Kikubwa ni kwamba sisikiki tu kwenye media hapa nyumbani. Ndiyo maana nimekuwa nikijaribu kufanya juu chini ili kurudi. Changamoto wakati mwingine ni menejimenti na wadau wa muziki kushindwa kutoa sapoti ipasavyo.

Risasi: Kimuziki kwa sasa umejikita wapi maana kuna wakati upo Bongo na wakati mwingine haupo?

 

Mr Nice: Sanasana nipo Kenya. Na ndiko ninapigia shoo za kufa mtu.

Risasi: Kwa nini shoo umekuwa ukifanya zaidi nje ya nchi kuliko hapa nyumbani?

Mr. Nice: Makazi yangu yapo huko zaidi. Ninaishi Kenya. Kwa hiyo hata shughuli zangu za muziki na biashara zangu zote ninazifanyia huko.

Risasi: Bado malipo kwako ni kama zamani kwenye shoo, maana kipindi cha nyuma unatajwa kuwa mwanamuziki uliyekuwa unaongoza kwa malipo makubwa?

 

Mr. Nice: Siku zote na miaka yote bei huwa ni maelewano. Unapozungumzia kulipwa zaidi kuna kipindi mtu anaweza kulipwa zaidi na wakati mwingine kipato kinaweza kikawa cha chini zaidi. Mambo yanabadilika.

Risasi Vibes: Unafikiri ukifanya kiki zinaweza kukurudisha kuwa mwanamuziki anayezungumziwa kama ambavyo wanafanya wasanii wengi kwa sasa?

Mr. Nice: Hapana. Kazi nzuri ndiyo ninaamini inaweza kunirudisha kuwa mwanamuziki mkubwa zaidi. Kiki si kitu na wanamuziki au wasanii wanaotegemea kiki kiukweli ninawadharau. Kimsingi kiki ni ujinga na ningependa jamii kwa ujumla wake ikemee masuala ya kiki maana yanatuharibia tasnia yetu ya muziki.

 

Risasi Vibes: Tutegemee nini kutoka kwako kwa sasa?

Mr. Nice: Mengi. Nipo jikoni ninajikita vizuri katika kazi. Nimefanya ngoma nyingi na prodyuza Eck wa Eck Production na ninatarajia pale ambapo nitaanza kuziachia kazi zangu, kufanya vizuri na kurudi pale ninapostahili. Hii nadharia kwamba nimepotea nafikiri itaisha.

Makala: Boniphace Ngumije, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.