Mshukiwa wa Mauaji ya Watu 10 Waliouawa kwa Kisu Canada Akutwa Akiwa Amefariki

MSHUKIWA mmoja wa mauaji ya watu 10 waliouawa kwa kuwachoma kisu anayeitwa Damien Sanderson mwenye umri wa miaka 31, amekutwa amefariki dunia katika Jimbo la Saskatchewan nchini Canada.
Polisi wa Canada wametoa taarifa hiyo na kueleza kuwa mwili wa mshukiwa huyo ulipatikana katika eneo la James Smith Cree Nation, nyumbani kwa waathiriwa kadhaa wa tukio hilo.
Polisi wamesema kuwa mshukiwa mwengine anayeitwa Myles Sanderson ambaye amehusika na mauaji hayo yaliyotokea hivi karibuni, anasadikika kuwa amejificha katika Jiji la Regina nchini humo.

Siku ya Jumapili, watu 10 waliuawa kwa kuchomwa visu nchini Canada ambapo tukio hilo limetajwa kuwa ni mojawapo ya matukio mabaya zaidi katika historia ya hivi karibuni katika taifa hilo.
Mashambulizi hayo ambayo yalisababisha watu wengine 18 kujeruhiwa katika Jimbo la Saskatchewan lililopo mashambani.
Taarifa zinaeleza kuwa familia za wahanga wa tukio hilo zipo katika maombolezo huku ikidaiwa mara ya mwisho washukiwa wa mauaji hayo walionekana katika Mji wa Regina.
Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao

