The House of Favourite Newspapers

Mtatiro Apania Kuipaisha Tunduru – Video

DC Julius Mtatiro ndani ya Studio za Global Radio.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro amesema amejipanga vilivyo kuipaisha wilaya hiyo katika nyanja mbalimbali kimaendeleo.

 

Kabla ya kujiunga na CCM na baadaye kuteuliwa kuwa DC, Mtatiro alikuwa Kada wa CUF ambapo alishika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo Katibu Mkuu na baadaye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, nafasi ambayo alikuwa nayo hadi pale alipoamua kuachana na chama hicho.

 

Akizungumza kwenye Kipindi cha Mwendokasi kinachorushwa na +255 Global Radio, leo  Ijumaa, Mtatiro alisema anatamani kuhakikisha anafanikisha malengo aliyojiwekea wilayani humo kabla muda wake wa kazi haujaisha.

Mtatiro na watangazaji wa Global TV, Lucas Masungwa (kushoto) na Abdallah Ng’anzi (kulia).

Akitaja vipaumbele vyake ambavyo ameanza navyo kwa mafanikio makubwa, alisema cha kwanza ni elimu –hasa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ‘mabazazi’ wanaoharibu ndoto zao kwa kuwapa mimba.

 

“Mimi na wenzangu pale wilayani tumejipanga vizuri kuhakikisha tunasimamia elimu vizuri. Kwa sasa tuna kampeni kubwa ya kuhakikisha watoto wetu wa kike wanaosoma sekondari wanakuwa na hosteli za kutosha.

“Mheshimiwa Rais akiniacha mwaka mmoja au miwili kutakuwa na hosteli za kutosha katika shule zetu,” alisema Mtatiro.

 

Katika kukazia hoja hiyo, DC Mtatiro aliitaja Shule ya Sekondari ya Masonya kuwa ya mfano kwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, sababu ikiwa ni wanafunzi wa kike kuishi bweni.

Mtatiro akiwa na Mkuu wa Vipindi wa Global Radio, Borry Mbaraka.

“Kama juzi tu hapa, wanafunzi walipimwa ujauzito, shule nzima ya Masonya hapakuwa na mtoto aliyekutwa na mimba. Niseme tu, huu ni mkakati wetu wa muda mrefu na tutalisimamia hilo,” alisema Mtatiro.

 

Mbali na elimu, Mtatiro alitaja mambo mengine wanayoyatazama kwa jicho la karibu kuwa ni kilimo cha korosho, ufuta na mazao mengine ya chakula.

Katika hatua nyingine, Mtatiro ambaye alipata kuwa Katibu wa Muungano wa Vyama vya Upinzani –Ukawa, alisema uamuzi wake wa kuhama CUF na kujiunga na CCM, ulisababisha matatizo kwake hadi kufikia hatua ya kutishwa.

 

“Nilitishwa sana, lakini sikujali. Ni jambo la kawaida, hata mheshimiwa Rais Magufuli wakati alipoingia madarakani yalisemwa mengi,  wengine walisema hakutakuwa na mabadiliko. Kifupi sikuhofia.

Mtatiro akizungunmza na Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho.

“Mimi ni Mkurya, sina hofu…lakini pia mimi ni Mkatoliki, tunasali muda wote, kwa hiyo sina hofu. Sikuwa na hofu na hata sasa sina hofu,” alisema.

Ili kusikiliza Global Radio kwa vipindi mbalimbali, ingia Playstore kwenye simu yako kisha pakua App ya 255 Global Radio.

Stori: Joseph Shaluwa

Comments are closed.