The House of Favourite Newspapers

Mtibwa: Adhabu Yetu CAF Ilishamalizika Kitambo

Kikosi cha timu ya Mtibwa Sugar.

UONGOZI wa Mtibwa Sugar umewataka wapenzi na mashabiki wa soka hapa nchini kuupuzia taarifa za kuwa hata kama ikifanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe laFA haitaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani kwa kile kinachodaiwa kuwa eti bado inatumikia adhabu yake ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

 

Mwaka 2003, Mtibwa Sugar ilifungiwa na CAF kutoshiriki michuano yoyote inayosimamiwa na shirikisho hilo kutokana na kushindwa kwenda kucheza dhidi ya Santos FC ya Afrika Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kile kilichodaiwa kuwa uongozi wa klabu hiyo ulikosa fedha za nauli za kuisafirisha timu hiyo kwenda nchini humo.

 

Hiyo ilikuwa ni baada ya mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo hapa nchini na Mtibwa Sugar kukubali kipigo cha mabao 3-0.

Akizungumza na Championi Juma, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema kuwa adhabu yao hiyo ilishaisha siku nyingi na amewataka wale wote wanaowapotosha mashabiki wao kuacha mara moja kufanya hivyo.

 

“Adhabu hiyo ilishaisha siku nyingi, kwani tulifungiwa miaka mitatu kutoshiriki michuano ya CAF, kutokana na kosa hilo la kutoenda Afrika Kusini kucheza na Santos, kwa hiyo wanasema bado tumefungiwa tunaomba waache mara moja kuwadanganya mashabiki wetu.

 

“Tangu kipindi hicho mpaka sasa ni karibia miaka 15 kwa hiyo ni wazi kuwa adhabu yetu ilishaisha na sasa tunajiandaa kuhakikisha mwaka huu tunakuwa mabingwa wa Kombe la FA ili tuweze kuiwakilisha Tanzania katika michuano Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya nne,” alisema Kifaru.

Mara ya kwanza kwa Mtibwa

Sugar kushiriki michuano hiyo ilikuwa mwaka, 2001, kisha ikashiriki 2002 na mara ya mwisho ilikuwa ni 2003, katika miaka hiyo yote ilikuwa ikishia hatua ya pili ya michuano hiyo.

Comments are closed.