Mtihani wa Congo na Misri utaivusha Simba

WAWAKILISHI pekee wa Ukanda wa Cecafa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni Simba ya Tanzania. Hakuna timu yoyote ya Afrika Mashariki iliyokuwa na pumzi ya kutinga hatua hiyo msimu huu zaidi ya Simba.

 

Imepangwa kundi moja na AS Vita ya DR Congo, JS Soura ya Algeria na Al Ahly ya Misri. Wikiendi iliyopita ilipiga mechi yake ya kwanza Jijini Dar es Salaam ikashinda mabao 3-0. Ni mwanzo mzuri kwa Simba kwenye hatua hiyo muhimu yenye heshima kwa klabu yoyote inayopenda maendeleo ndani na nje ya uwanja.

 

Hiyo inamaanisha kwamba inaongoza kundi lake na leo inakwenda Congo kucheza na Vita Jumamosi usiku jijini Kinshasa. Simba ina mechi mbili ngumu za ugenini ambazo kimahesabu ni mtihani mkubwa ambao wakiweza kuucheza vizuri zitawajengea heshima kubwa na kuwasogeza hatua ya robo fainali. Simba ikitoka Kinshasa itakwenda Misri kukipiga na Ahly.

 

Ni mechi nyingine ngumu ingawa Simba ina kikosi kipana ambacho kiufundi kinaweza kutengeneza matokeo ndani na nje ya nchi. Simba kama wawakilishi wa nchi wanahitaji sapoti kubwa ya kila mdau ndani na nje ya uwanja ili kufanya vizuri kwenye michezo hiyo muhimu.

 

Kila mmoja anapaswa kuelewa uwekezaji mkubwa uliofanywa na wapinzani hao wa Simba haswa kwa kuzingatia kwamba walishawahi kucheza fainali mara kadhaa na wanaelewa utajiri uliopo. Maoni yetu ni kwamba Simba wajitahidi kukaza kwa kila linalowezekana kuhakikisha wanapata angalau sare mbili kwenye mechi hizo ili kujiweka pazuri zaidi na kufanya maajabu msimu huu.

 

Kuna changamoto za hapa na pale kwenye nchi za Congo na Misri, Simba inapaswa kujiandaa kisaikolojia kuweka mambo yao sawa. Maandalizi ya mapema ni muhimu nje ya uwanja kwa kuweka sawa miundombinu kama viwanja na mambo mengine ili kuepuka sababu ambazo hazina msingi, wawakilishi wetu wafanye maandalizi mapema ili kuepuka visingizio ambavyo tumekuwa tukivitoa mara kwa mara ugenini ambazo sidhani kama vinasaidia.

 

Kila mmoja anapaswa kujua kwamba kutokana na umuhimu wa mashindano hayo kila mwenyeji
anajitahidi kuhakikisha kwamba anabeba pointi zote nyumbani ili kujiweka kwenye mazingira mazuri kwa vile anajua ugumu wa ugenini, ndiyo maana tunasihi maandalizi ya mapema ili kuepuka visingizio. Hakuna lisilowezekana kwenye soka haswa pale inapowekwa nia kwa wachezaji, viongozi na mashabiki na miundombinu ikakaa sawa kila mmoja akafanya kazi yake kwa nafasi yake.

 

Soka limebadilika mafanikio yanakuja kutokana na juhudi na uwekezaji kama ambao Simba wameanza kuufanya, ni wakati mzuri kwa mashabiki kushikamana zaidi kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Vilevile kama wadau watapambana kuisaidia Simba kutamuongezea zaidi morali wa kuwekeza Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye ufanisi wake utavutia watu wengine na kuboresha soka la Simba na masilahi mapana ya Tanzania. Tuisapoti Simba ivuke mitihani miwili ya ugenini.

Loading...

Toa comment